Kauli hiyo ya Dk. Mwakyembe imekuja siku chache baada ya kusambazwa kwa
waraka unaodaiwa kuandikwa naye, ukimuhusisha na tuhuma za kumshambulia
Lowassa, jambo ambalo amelifananisha kuwa ni sawa na siasa za kitoto.
Akizungumza jana katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na
kituo cha redio Clouds FM, alisema kutokana na kusambazwa kwa waraka
ambao umeandikwa nyadhifa zake za ubunge na uwaziri, hivi sasa
ameshaanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu waliokuwa
wakiusambaza.
Waziri Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwanahabari, alisema
anapata shaka hata na baadhi ya vyombo vya habari pamoja na mitandao
hiyo na kudai kuwa anamshambulia Lowassa.
“Ninashangazwa sana na hii mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya
habari (magazeti), vimekuwa vikiandika vitu vibaya ikiwa ni pamoja na
kumshambulia Lowassa wakati hata siku moja sijazungumza nao.
“Kitendo cha baadhi ya watu wa aina hii kuwaandika vibaya wanasiasa
katika mitandao ya kijamii kwa kutumia majina ya watu wengine ni ishara
ya woga wa kisiasa na kushindwa kujiamini katika misimamo yao.
“…Kinachonikera kupindukia ni kuwa taarifa hizo sijawai kuziandika ila
kuna mtu ama kundi maalumu la watu limeziandika na kuweka jina langu na
nafasi zangu za uongozi kama mbunge na waziri, huu si uungwana na wala
si siasa kwa kuchezea majina ya watu. Kama siasa zimefika huku basi ni
za hatari,” alisema.
Dk. Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela mkoani Mbeya, alisema katika
kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, watu wanapaswa kuacha woga na
kutojiamini.
“Kitendo cha kutumia majina ya watu na kuelezea hisia zao ni kukosa
ujasiri na hata yanayosambazwa kwenye mitandao hayaendani na hadhi yangu
kiongozi, sina tabia ya woga na uongo,” alisema.
Alisema baada ya kupata taarifa zilizopo mitandaoni alilazimika kutoa
taarifa kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Makosa ya Mtandaoni pamoja na
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kulalalimikia mchezo huo
mchafu.
Dk. Mwakyembe alisema vyombo hivyo vimeshaanza uchunguzi mkali ili kuwabaini watu walioandika na kutuma taarifa hizo.
“Hizo porojo zilianza tu polepole, zilienda mitandao ya kijamii na
magazeti kuwa nimesema Lowassa hana sifa ya kuwa rais, wengine walisema
niliwaambia nitapambana kufa na kupona Lowassa asiingie Ikulu wakati
sijaongea nao na sijawahi kusema, huu ni mchezo wa kitoto uliopitiliza,
lakini una madhara makubwa,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema kutokana na hali hiyo, amedhamiria na kuhakikisha kesi ya kwanza
ya matumizi mabaya ya mitandao inaanzia kwake kwa kuwa hana utamaduni
wa woga, na watu wanapaswa kuwa wazi endapo wanakuwa na vitu na si
kutumia majina ya watu.
Dk. Mwakyembe alisema anashangazwa na watu kutumia jina lake kumchafua
kwa kuwa hana tatizo na mtu yeyote na kama chanzo ni suala la Richmond,
ilikuwa ni kazi aliyopewa na Bunge.
Alisisitiza kuwa alifanya kazi hiyo vizuri kwa kumuweka Mungu mbele, lakini si kuongea uongo jambo ambalo si utamaduni wake.
“Wananchi wanapaswa kutambua kuwa nchi inaendeshwa kisheria na ninaamini
wahusika wote waliofanya tukio hilo watachukuliwa hatua za kisheria,”
alisema.
Umoja wa Ulaya Nao Wakanusha;
Jana Umoja wa Ulaya (EU) ulikanusha vikali kwamba balozi wake
nchini alifanya mkutano na waandishi wa habari na kumtahadharisha Rais
Jakaya Kikwete kwamba nchi yake inaweza kuingia matatani na EU kama
Lowassa atateuliwa kuwa mgombea urais kupitia CCM.
Ofisa Habari wa EU, Susanne Mbise jana alikanusha taarifa izo na kusema kuwa hata wao wamesikia taarifa hizo, lakini ukweli wa jambo hilo upo kwenye taarifa waliyoweka kwenye mtandao wa Face Book ya Umoja huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa anayeshughulikia Siasa na Habari, Luana Reale wa kitengo cha habari, Balozi huyo hajafanya mkutano wowote na mwandishi yeyote na kwa maana hiyo hajatoa taarifa yoyote kwa vyombo vya habari.
Reale alisema kuwa tangu Juni mosi mwaka huu Balozi huyo hayuko nchini kwani alisafiri kwenda makao makuu ya Umoja huo na hajarejea nchini.
Alisema kuwa EU ina uhusiano mzuri wa muda mrefu na Tanzania ambao umejengwa juu ya misingi ya kuheshimiana na kuaminiana.
EU inatoa taarifa hizo baada ya watu wasiojulikana kusambaza taarifa za uzushi na uongo kwenye mitando ya kijamii wakidai kuwa Rais Kikwete ameonywa kwamba Lowassa akipitishwa kuwania urais uhusiano wa Tanzania na EU utaingia shakani na kwamba hawataisaidia katika miradi ya maendeleo.
Wazushi hao walidai kuwa Lowassa ni mtuhumiwa namba moja wa rushwa nchini na kutaja kuwa anahusika katika kadhia ya Richmond na NIC.
Na Mpekuzi blog
Post a Comment