Dk Slaa alisema, kauli hiyo ni moja kati ya nyingi
zinazotolewa na viongozi wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambazo
Watanzania wamechoka kuzisikia na badala yake wanahitaji vitendo.
Alitoa kauli hiyo juzi mjini Tunduma wilayani
Momba mkoani Mbeya, alipokuwa akihutubia wakazi wa mji huyo katika
mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Tunduma.
Dk Slaa alisema Watanzania wanahitaji safari yenye
uhakika wa maendeleo ambayo watayapata Oktoba, mwaka huu, kupitia
upinzani lakini siyo kutoka kwa kiongozi yeyote wa CCM.
“Eti safari ya matumaini, hivi kweli Tanzania
iliyojaa kila aina ya madini na utajiri wa kutisha halafu tunasema
safari ya matumaini badala ya vitendo? Watanzania tumechoka na kauli za
matumaini, tumechoka kuishi kwa matumaini katika nchi yetu,” alisema Dk
Slaa.
Mbali na hilo, Dk Slaa aliwashangaa baadhi ya
watangaza nia wa CCM walioiponda Serikali yao kwamba imeshindwa wakati
wao ndio walitakiwa kuwa mstari wa mbele kuondoa kero hizo.
Ukawa wajipanga
Akizungumza kuhusu Ukawa walivyojipanga kuingia
Ikulu Oktoba mwaka huu, Dk Slaa alisema wana akiba ya kutosha ya
viongozi makini wa kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
Alisema wakishika dola hawatakuwa na sababu yoyote ya kukopa viongozi kutoka kwa CCM.
“Hatuna njaa ya viongozi ndani ya upinzani, tunao
wa kutosha. Hatuna haja ya kwenda CCM kuwakopa viongozi, Oktoba tupeni
ridhaa upinzani tubadili sura ya nchi,” alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbozi Magharibi
(Chadema), David Silinde alisema, licha ya Serikali ya CCM kuamua kugawa
majimbo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujiokoa,
hawataambulia kitu kwani wamejipanga kukabiliana na hali yoyote
itakayojitokeza.
“CCM tumewagundua na janja yao, baada ya kuona
wabunge wao wamekabwa koo, ndio wanatafuta njia mbadala ya kujiokoa kwa
kugawa majimbo, lakini tunasema majimbo yote yaliyopendekezwa kugawanywa
Mbeya kama yatapitishwa tunachukua yote,” alisema Silinde.
Post a Comment