Dk Willibrod Slaa.
Wakati kukiwa na taarifa zinazosambaa mtandaoni zikimuhusisha Dk
Willibrod Slaa na akaunti ambayo imekuwa ikitoa msimamo wake wa
kujitenga na shughuli za siasa pamoja na Ukawa, katibu huyo mkuu wa
Chadema amekanusha taarifa hizo akisema hajawahi kuwa na akaunti ya
twitter.
Hii ni mara ya pili kwa Dk Slaa kuzungumza akikatakaa kufafanua
mambo mbalimbali yanayohusu sakata lake na Chadema, akiahidi kuwa
kufanya hivyo baadaye, huku akiweka bayana kuwa hajawahi kuwa na akaunti
ya twitter.
Dk Slaa, aliyekuwa anatajwa kuwa mgombea urais wa Chadema,
hajaonekana hadharani katika matukio makubwa ya kichama tangu Chadema na
Ukawa walipomkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumteua
kuwa mgombea urais anayeungwa mkono na vyama vinne vinavyounda umoja
huo.
Mara ya mwisho kuonekana kwenye shughuli za chama hicho ni katika
kikao cha Kamati Kuu wakati Lowassa alikaribishwa kufanya majadiliano na
kujibu hoja za wajumbe.
Lakini baada ya hapo Dk Slaa hakuonekana wakati wa kutambulishwa kwa
Lowassa kwa waandishi wa habari, tukio la kuchukua na kurudisha fomu za
urais ndani ya chama na tukio la juzi la kuchukua fomu za urais kutoka
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wakati hayo yakiendelea, kuna akaunti ya twitter yenye jina la “Dr
Willibrord Slaa” ambayo imekuwa ikitoa kauli mfululizo zikiwa na ujumbe
mbalimbali unaoendana na mazingira aliyomo sasa mwanasiasa huyo.
Agosti 10, kulitumwa ujumbe zaidi mara 10, mmojawapo ukijaribu kuwaaminisha watu kuwa hiyo ni akaunti halisi ya Dk Slaa.
“Ndugu zangu Watanzania, hii ni akaunti yangu rasmi, bila shaka
yoyote na naomba ninachoandika hapa kifikishwe kwa Watanzania popote
walipo,” unasema ujumbe huo.
Taarifa nyingine zilizotumwa kwenye akaunti hiyo ya twitter ni pamoja
na ile iliyoeleza kuwa Dk Slaa ameomba ulinzi kutoka nchi na
mashirika ya kimataifa na atazungumza kupitia runinga na redio pindi
atakapopata ulinzi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Slaa alisema hajawahi kutuma taarifa yoyote kwenye mitandao ya kijamii.
“Sijawahi ku-operate (kuendesha) kitu chochote kwenye akaunti ya twitter, sina akaunti kama hiyo,” alisema Dk Slaa.
Mbali na kukanusha kumiliki na kuendesha akaunti hiyo, Dk Slaa
alirudia kauli yake ya wiki iliyopita kuwa atatoa msimamo wake muda
muafaka utakapofika, baada ya kuulizwa swali kuhusu hatma yake ndani ya
Chadema na kisiasa kwa ujumla.
“Subira yavuta heri, sasa ili uipate hiyo heri unatakiwa kuvumilia.
Kwa hiyo wakati ukifika nitazungumza tu na Watanzania,” alisema.
Alipoulizwa ni wapi alipo kwa sasa, alisema yupo Dar es Salaam
anapumzika, lakini akasisitiza kuwa ipo siku ataweka wazi mustakabali
wake kisiasa.
Dk Slaa alisema yeye na mke wake Josephine Mushumbusi wanatarajia
kusafiri kwenda nje ya nchi katika siku chache zijazo, ingawa hakuweka
wazi nchi anayotarajia kuitembelea, lakini akasema atarejea baada ya
wiki moja.
(CREDIT: MWANANCHI)
Post a Comment