Mara nyingi wamekuwa wakieleza namna wanavyoweza kuwapatia manufaa wananchi kama watawachagua, mfano kuhakikisha wanapata maji safi, barabara bora na vinginevyo.
Wanasiasa wanajulikana kwa kutotekeleza ahadi zao na wengi wao wamekuwa wakishindwa kuzitekeleza kwa kutoonekana kabisa baada ya kupewa kura
Halafu, wanaonekana kipindi kama hiki cha uchaguzi kwa kuwa kwa mara nyingine wanataka kupata kura, yaani wachaguliwe tena.
Kabla ya uchaguzi mkuu ambao unatarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu, huenda wanasiasa wanaweza kujifunza kupitia Yusuf Said Bakhresa.
Yusuf ambaye ni mmoja wa wamiliki wa klabu ya Azam FC na Azam Media Group inayomiliki Azam TV, ameamua kumwaga takribani Sh milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa barabara jijini Dar es Salaam.
Yusuf ambaye ni wakala wa kuuza wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), tayari ameishajenga mitaa miwili na anatarajia kujenga mingine miwili.
Mitaa yote ipo katika eneo la Msasani jijini Dar es Salaam, karibu kabisa na yalipokuwa makazi ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ujenzi wa barabara hizo umefanywa na wataalamu wa Kichina ambao badala ya kutumia lami kama ilivyozoeleka, Wachina hao wamejenga kwa kutumia saruji, wakitupia zege lenye unene mithili ya mikate mitatu iliyobebana!
Ujenzi huo umeanzia kwenye mtaa unaotokea katika barabara ya Mwai Kibaki, unaingia hadi kwenda kukutana na mtaa uliopewa jina la Ngome Road.
Mtaa huo ndiyo kuna makazi ya milionea huyo upande mmoja akiwa amepakana na kampuni maarufu ya upangishaji nyumba za kisasa ya Blue Mark.
Pamoja na kutengenezwa kwa ubora wa hali ya juu, milionea huyo amehakikisha mitaa hiyo miwili imewekewa taa na ing’ara kama New York.
Huenda ndiyo mitaa miwili pekee inayoingia kutoka barabara kubwa yenye taa nyingi kuliko yoyote ile jijini Dar es Salaam na Tanzania nzima.
Taa zake pia huenda ndiyo ghali kuliko zote zilizo katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam kwa kuwa zinatumia mfumo wa solar, hazitegemei umeme wa Tanesco ambao hauna uhakika, maana unaweza kukatika wakati wowote.
Kama hiyo haitoshi, imeelezwa bajeti hiyo ya Sh milioni 400 itatumika kuitengeneza mitaa mingine miwili ya Barakani Road na mwingine mdogo unaounganisha Barakani Road na Ngome Road.
Ingawa wanaoishi katika maeneo hayo wengi ni vigogo, imeelezwa Yusuf aliwachangisha kiasi kidogo cha fedha ambacho huenda hakifiki hata asilimia 20 ya alichotoa.
“Alichofanya ni kama kutaka kuonyesha ujirani, yaani ajue anashirikiana na watu wanaoishi karibu yake. Lakini fedha zote anatoa yeye na hatua ya pili ni kujenga tena mitaa hiyo miwili,” alieleza rafiki wa karibu wa Yusuf ambaye ni mmoja wa watoto wa bilionea namba moja Tanzania na Afrika Mashariki, Said Salim Bakhresa.
Juhudi za kumpata Yusuf alizungumzie suala hilo zilikwama baada ya kuelezwa yuko safarini nje ya nchi kikazi.
Lakini taarifa za uhakika zinaeleza, hana mpango wa kugombea udiwani wala ubunge, badala yake alifanya hivyo kama mchango wake kwa jamii na kuboresha mazingira ya eneo hilo analoishi pamoja na majirani zake.
Post a Comment