APRILI 7 mwaka 2012 tasnia ya filamu ilipatwa na majonzi makubwa
kutokana na kifo cha aliyekuwa mwigizaji nguli, Steven Kanumba, ambaye
alikuwa kipenzi cha wengi ndani na nje ya nchi.
Licha ya wengi kutokuamini kwa muda huo, baada ya muda ikagundulika
kweli amefariki, hivyo majonzi zaidi yakarindima, huku kila mtu akisema
lake kuhusu kifo hicho.
Baada ya mazishi yake mashabiki walijipa matumaini kwamba tasnia hiyo
licha ya kumpoteza mwigizaji huyo ingeendelea vema kutokana na kuwa na
idadi kubwa ya waigizaji wenye sifa kama za Kanumba, lakini hadi leo
mwaka wa tatu tasnia hiyo inaonekana kupoteza mvuto.
Mwigizaji, Yobnesh Yussuf ‘Batuli’, alipotembelea Kampuni ya New Habari
(2006) Ltd , aliongeza chachu ya kutaka kujua zaidi anamkumbukaje
Kanumba ambaye waliwahi kufanya kazi kwa ukaribu.
“Wasanii wengi hatujui tatizo ni nini, ndiyo maana naweza kusema kama
ameacha laana kwa kuwa tumekutana mara kwa mara kuzungumzia jambo hilo,
lakini kama tumeshindwa tumejitahidi na hakuna aliyeweza kufikia mvuto
na uwezo wake kwa mashabiki, ndiyo maana tunaonekana kama tunapoteza
mwelekeo na kifo chake ni kama kimeacha laana kwa filamu za Tanzania,’’
anaeleza Batuli.
Batuli, mwenye watoto wawili ambaye amezaa mapema kwa hofu ya uzuri wake
kuisha kabla ya kupata motto, anasema wakati mwingine wanajikuta
wakisema kwamba kwa sasa wanasubiri muujiza ya Mungu ndiyo kutokee
mapinduzi mapya katika filamu za bongo, maana kwa sasa hali imeyumba.
Tatizo nini?
Batuli anasema zipo changamoto nyingi zinazowafanya wasifikie mafanikio
aliyokuwa nayo Kanumba katika filamu, likiwemo la kutokuaminiwa na
wafadhili kunakotokana na baadhi ya waigizaji maarufu wenye majina
makubwa katika tasnia hiyo kudhulumu wafadhili hao kiasi kwamba hawataki
kufanya kazi na waigizaji wengine wa filamu.
“Wapo wafadhili wameshatoa fedha nyingi kwa baadhi ya masupastaa wetu
ili watengeneze filamu zenye ubora na kiwango cha juu ili kuleta hamasa
katika soko la filamu kama ilivyokuwa enzi za Kanumba, lakini hakuna
aliyethubutu hadi leo, wengi wao wametumia kwa maslahi ya pombe, mapenzi
na mambo mengine, wamesahau kwamba walipewa fedha kwa ajili ya kufanyia
mapinduzi ya filamu,’’ anaeleza.
Licha ya hayo, Batuli bado anaamini kwamba Kanumba alikuwa na vitu vingi
vya ziada vilivyomfanya apendwe ndani na nje ya nchi, vikiwemo uthubutu
wake, kujitambua na kuwa na uchungu wa mafanikio.
“Kanumba alikuwa hakurupuki, alikuwa hakati tamaa, hata alipokuwa
akichekwa aliamini ipo siku atapigiwa vigelegele, alikuwa mbunifu na
mpenda kukosolewa asiye na woga wa kufanya lolote analoona ni fursa
kwake,’’ anaendelea kumuelezea.
Anasema: “Kuna kipindi alikuwa anajipanga kwenda kuigiza na waigizaji wa
Nigeria, aliponiambia mpango wake huo nilicheka kwamba anakwenda huko
ataongea Kiingereza gani, lakini sikuamini jibu lake alisema watajua
huko huko, kweli alikwenda na akaigiza na waigizaji wa Nigeria ambao ni
maarufu.
“Nakumbuka tulikuwa tukikutana naye kwenye masomo ya Kiingereza,
alipokwenda Big Brother watu walicheka Kiingereza chake, lakini hakukata
tama, alizidi kujifunza na kujituma, hatimaye akacheza filamu ya
“Moses” na mwigizaji maarufu nchini Nigeria, Ramsey Noah, tena kwa
Kiingereza kizuri, kila mmoja akaikubali filamu hiyo na ujio wake wa
kutangaza soko kimataifa,’’ anaeleza Batuli huku akidai kwamba ni vigumu
kuziba pengo la Kanumba.
Haki miliki
Akizungumzia haki miliki, Batuli anaeleza kwamba ni jambo baya
linalowaumiza wasanii kwa kuwa baadhi ya wasambazaji wananunua
hakimiliki za wasanii, hivyo wakifariki dunia hukosa haki zao nyingi za
msingi.
“Mfano mzuri ni kwa Kanumba, kama kungekuwa na hakimiliki ya kazi zake
nadhani filamu zake zingeendelea kuuzwa na fedha zingesaidia familia
yake, lakini nadhani kwa sasa hali si hivyo, ushauri wangu ni kwamba
wanunuaji wa kazi za wasanii wasinunue hakimiliki za kazi zao ili
wawasaidie kupiga hatua ya kimaendeleo,’’ anaeleza.
Mapenzi
Batuli anasema alikuwa anafahamu kwamba mwigizaji mwenzake, Nice Mohamed
‘Mtunisi’ alikuwa akimpenda muda mrefu lakini alikuwa mzito kumtamkia.
“Mtunisi aliniogopa, domo zege, wajanja walimuwahi lakini baada ya
kusikia nimeachana na mume wangu wa mwanzo akaja kwa gia zote,
nikamkubali tukawa wapenzi, lakini hatukupata mtoto,” anaeleza.
“Lakini kwa muda wote wa miaka miwili ya mapenzi yetu alikuwa akinitenda
mno, alinidanganya mengi, ilifika kipindi aliniletea dada wa ndani
kumbe ni mke mwezangu, nilipochunguza nikagundua kwamba ana mke
aliyekuwa akiishi Kimara na pia nilisikia tetesi za kuwa na uhusiano wa
kimapenzi na mwanamuziki, Pauline Zongo, nilipomuuliza alikataa.”
Anasema anakumbuka maisha ya Mtunisi kama maigizo, hakuwahi kumwambia
kama alikuwa na mke, lakini alipofanya uchunguzi wake akagundua kwamba
alikuwa na mke Kimara, alipomfuatilia yule mwanamke akaja moto akiwa na
gazeti lake lililoandikwa habari zangu kuhusu Mtunisi, lakini baada ya
kumtuliza na kuzungumza, tukatambua kwamba mwanamume huyo alikuwa
akituchezea bila kujijua.
“Mtunisi alikuwa ndani, alipotoka akanipiga kibao, akidai nimekwenda
kumfanyia fujo, hapo akaongeza hasira, mimi na yule mwanamke wake
tulimchangia tukampiga sana, hatasahau na mapenzi yakaishia hapo, kila
mtu akawa na maisha yake sina cha kukumbuka, zaidi najutia kupoteza muda
wangu kwake,’’ anaeleza Batuli.
Kuasili watoto
Akielezea maisha ya kuwa na watoto zaidi, anasema anatamani watoto zaidi lakini wa kike tena wawe mapacha.
“Napenda mtoto wa kike kwa kuwa nina watoto wawili wa kiume, nitazungumza na wataalamu wa masuala ya uzazi kama nitafanikiwa sawa lakini nikishindwa nitaasili mtoto wa kike,’’ anaeleza.
“Napenda mtoto wa kike kwa kuwa nina watoto wawili wa kiume, nitazungumza na wataalamu wa masuala ya uzazi kama nitafanikiwa sawa lakini nikishindwa nitaasili mtoto wa kike,’’ anaeleza.
Gazeti la Mtanzania,22 May 2015
Post a Comment