Ni wiki ya mtikisiko. Hivi ndiyo unavyoweza kuelezea hali itakavyokuwa nchini kutokana na matukio makubwa ya kisiasa yanayotazamiwa kutokea ndani ya wiki inayoanza leo ambayo yanaweza kubadili mwelekeo wa siasa za Tanzania.
Hali hiyo
inatokana na vuguvugu la kisiasa linalohusisha viongozi wenye ushawishi
kuhama vyama vyao vya siasa na kutimkia kwenye vyama vingine, ikiwa ni
siku chache kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Ni
wiki ambayo itapambwa na matokeo ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi wa
CUF kilichofanyika jana mjini Zanzibar kuhusu mustakabali wake ndani ya
Ukawa, ikizingatiwa kuwa hivi karibuni chama hicho kiliamua kujiweka
kando ya vikao vya umoja huo hadi vikao vya juu viamue.
Hata
hivyo, habari ambazo tumezipata zinasema kuwa uwezekano wa
chama hicho kujitoa ndani ya Ukawa ulikuwa mdogo kutokana na kuogopa
hasira za wananchi wenye matumaini na umoja huo.
Aidha,
kulikuwa na taarifa kuwa kikao cha jana kilikuwa kinaangalia jinsi
watakavyoshiriki katika umoja huo na kwamba kulikuwa na matumaini
makubwa.
Vile vile, hii ni wiki ambayo kura za maoni
zinazoendelea katika vyama vikubwa vya siasa, kuonyesha baadhi ya vigogo
wakiangushwa na kujaribu kutafuta upenyo wa madaraka katika vyama
vingine.
Pia, ni wiki ambayo chama kikuu cha upinzani,
Chadema kimeamua kusogeza mbele tarehe za kuchukua na kurejesha fomu za
kuomba kuteuliwa kugombea urais kutoka jana hadi Ijumaa, katika kile
kinachotazamwa kama kusubiri mchakato wa kumpata mgombea urais.
Kana
kwamba hiyo haitoshi, hii ni wiki ambayo minong’ono ya waziri mkuu wa
zamani Edward Lowassa ambaye jina lake limekatwa katika orodha ya wasaka
urais wa CCM anaweza kuhamia Chadema.
Tayari baadhi ya
viashiria vya hali hiyo vimeanza kuonekana ambapo wiki iliyopita
wabunge wawili wa chama tawala cha CCM, James Lembeli na Ester Bulaya
waliachana na chama hicho na kujiunga na Chadema huku chama hicho cha
upinzani kikitamba kujiandaa kuwapokea vigogo wengine zaidi.
Kiashiria
kingine cha mtikisiko ni hatua ya madiwani 18 wa CCM wilayani Monduli
na wengine 10 wa UDP na CCM Bariadi kuhamia Chadema.
Lakini pia wapo wabunge na madiwani wanaohama Chadema kwenda chama cha ACT-Wazalendo.
Vuguvugu
hilo la kisiasa limekolezwa na kauli za wanasiasa wawili vijana kwa
nyakati tofauti, Godbless Lema na Zitto Kabwe kuwa wiki hii itakuwa ya
mshikemshike kutokana na mambo yaliyopangwa kufanyika.
Zitto: Ni wiki ya mabadiliko
Akiandika
kwenye kurasa zake za Facebook na Twitter jana, Zitto alisema, “Wiki ya
kuanzia Jumatatu tarehe 27 Julai 2015 itashuhudia mabadiliko makubwa
sana kwenye siasa za Tanzania. Kuimarika kwa mfumo wa vyama vingi vya
siasa ni jambo jema kwa nchi yetu.”
Alipotakiwa
kufafanua kauli yake, Zitto hakutaka kutaja matukio husika, lakini
alisisitiza kuwa mtikisiko wa kisiasa utatokea na mazingira ya hali hiyo
yataanza kubadilika kuanza kesho.
“Na huu ujumbe nilioandika hauna uhusiano na chama cha ACT-Wazalendo,” alisema.
Alipotakiwa kufafanua zaidi, alisema “Watanzania wasubiri mabadiliko ya siasa za Tanzania.”
Lema asema ni mtikisiko
Kwa
upande wake Lema, akiwa jimboni kwake Arusha, alisema wiki hii itakuwa
ya mtikisiko kwa CCM kwa sababu zaidi ya viongozi wake 950 kuanzia ngazi
ya kata, wilaya, mkoa na taifa watahamia Chadema.
Akizungumza
wakati wa kuwapokea vigogo watatu na wanachama 30 kutoka CCM jana, Lema
alisema kuanzia kesho kimbunga cha viongozi na wana CCM kuhamia Chadema
kitavuma kila kona ya nchi.
Vigogo hao ni Diwani wa Kata ya Moshono, Paul Matthysen na mwenyekiti wa CCM Kata ya Terat, Simon Mollel wote wa jijini Arusha.
Haya
yametokea ikiwa ni siku chache baada ya katibu mwenezi wa CCM wilaya ya
Longido, Tostau Mollel kahamia Chadema, huku baadhi ya watiania wa
udiwani na ubunge waliokamilisha maandalizi wakikacha kuchukua fomu za
chama hicho.
Miongoni mwa waliokacha kuchukua fomu bila
kutoa sababu ni mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye,
mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Arusha, Robinson Meitinyiku, mjumbe wa
Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, Mathias Manga na mwenyekiti wa CCM
mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole, wote wakitajwa kuwa kwenye timu ya
Lowassa.
“Hii iliyoanzia Bariadi, Monduli, Longido na
Arusha mjini ni mvua za rasharasha. Masika yataanza wiki ijayo (kuanzia
kesho Jumatatu) kwa zaidi ya viongozi 950 wa ngazi mbalimbali
watakapohama CCM na kujiunga Chadema,” alisema Lema.
Alifananisha
Chadema na kanisa au msikiti akisema milango yake iko wazi kuwapokea
wanachama wa vyama vingine wanaotaka kutumikia umma kujiunga nacho kwa
kutubu makosa yao na kusamehewa kabla ya kuingia kazini Oktoba 25, mwaka
huu.
Wabunge wanne Chadema watua ACT
Wakati
upepo ukivuma kutoka CCM kwenda Chadema, hali kama hiyo imekinufaisha
chama kipya cha ACT-Wazalendo baada ya kuvuna wabunge watatu wa viti
maalumu na diwani mmoja kwa mpigo kutoka Chadema.
Wabunge
hao ni Mhonga Ruhwanya (Kigoma), Chiku Abwao (Iringa ) na
AnnaMaryStella Mallac (Mpanda) wote kutoka Chadema, huku mwingine ambaye
jina lake tunalihifadhi kwa kuwa hatukumpata, akitimkia CCM.
Wabunge
hao wanaungana na Mbunge wa Kasulu mjini, (NCCR – Mageuzi ) Moses
Machali aliyehama kutoka NCCR-Mageuzi kwenda ACT Wazalendo, hivi
karibuni.
Akizungumza na mwandishi jana, Zitto alisema atawatangaza wakati wowote wabunge wengine sita kutoka CCM, Chadema na CUF.
Kauli ya Chiku Abwao
Akizungumza
kwa simu akiwa India, Abwao alikiri kuhamia ACT-Wazalendo akidai
kutoridhisha na mwenendo wa Chadema na hasa taarifa anazosikia za
Lowassa ambaye amekuwa akituhumiwa mambo mbalimbali kuhusishwa na
Chadema.
“Mimi kwa historia yangu kitu kilichonipeleka
upinzani ni kutafuta haki uwajibikaji na kupinga vitendo vya ufisadi na
rushwa, lakini nimekishangaa chama changu katika suala hili,” alisema.
“
Licha ya mambo ya sintofahamu yanayoendelea Chadema lakini hili la
Lowassa kama kweli atajiunga na chama hiki basi suala litakuwa ni moja
tu, ni chaneli ya kuingia Ikulu, lakini haya mambo mimi siyapendi kwa
sababu ni mtu wa kupinga ufisadi na kupigania haki za wanyonge,” alisema
Abwao
Alisema ameamua kuhamia ACT-Wazalendo, kwa
sababu ni chama pekee kitakachowakomboa Watanzania na kwamba ataenda
moja kwa moja kugombea jimbo la Iringa Mjini badala ya Isimani.
“Niliamua
kwenda Isimani kipindi kile ili kuijenga Chadema, lakini safari hii
nipo huku ACT-Wazalendo nitaenda kupambana na Mchungaji (Peter) Msigwa
na yeyote yule atakayepitishwa na CCM,” alisema Abwao.
Mhonga: Ni uamuzi tu
Mhonga
Rhuwanya alipouliwa alijibu kwa kifupi, “Kama ulivyosikia ndiyo hivyo
hivyo, mimi ni mtu mzima na nina maamuzi yangu kwani chama siyo dini.”
Alipoulizwa
atagombea ubunge kupitia ACT-Wazalendo, alijibu, “Kwani mtu akihamia
chama kingine ni lazima agombea ubunge… hata hivyo naweza kugombea
tena.”
Mallac aenda kupokewa
Kwa upande wake, Mallac alisema alikuwa safarini kwenda Katavi kupokewa ACT-Wazalendo.
“Niko
njiani naelekea Katavi mkoani kwangu kupokewa rasmi na kiongozi wangu
wa chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe,” uliosomeka ujumbe mfupi wa
maneno.
Zitto awapokea
Zitto
alisema huo ni mwendelezo wa chama hicho kuwapokea wabunge kutoka
katika vyama mbalimbali na hivi karibuni atawapokea wengine katika mikoa
ya Kagera, Tabora, Rukwa na Zanzibar.
“Tabora wako
wawili na Kagera mbunge mmoja wote wa CCM, kutoka wilaya ya Karagwe, pia
Zanzibar wawili kutoka CUF na Chadema. Hawa wote wanasubiri mchakato wa
kura za maoni umalizike ndipo tuwatangaze.
“Hawa
wabunge tuliowapokea ni sawa na asilimia 10 kati ya 50 niliosema, maana
watu walikuwa wananiuliza, ‘Zitto ulisema utawapokea wa kiasi kadhaa
mbona kimyaa?’ mambo ndiyo yameanza sasa.”
Diwani Chadema atua ACT
Katika
hatua nyingine, aliyekuwa diwani wa Kata ya Segerea (Chadema), Azuri
Mwambagi amejiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ya uhusiano mbaya kati
yake na viongozi wa Chadema wa jimbo hilo.
Mwambagi
alisema kuwa amekuwa diwani wa kata hiyo kwa miaka mitano lakini
hakukuwa na ushirikiano mzuri kati yake na uongozi wa jimbo hilo.
“Kila
ninachokifanya wenzangu wanasema sijafanya kitu na wanaamua kunizunguka
kwa wananchi, hali hii imenichosha,” alisema Mwambagi.
Katibu
wa jimbo hilo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Anna alisema hata
yeye amezisikia taarifa za diwani huyo kuhamia ACT- Wazalendo, lakini
akakana kuwapo mizengwe aliyofanyiwa Mwambagi.
“Tupo
katika mchakato wa kura za maoni na yeye ameomba kuteuliwa kugombea
udiwani Kata mpya ya Liwiti, kama anahisi alikuwa kiongozi bora enzi za
utawala wake kwa nini asisubiri matokeo ya kura za maoni ndipo afanye
uamuzi huo?” alihoji Anna.
(Imeandikwa na Bakari Kiango na Peter Saramba-Mwananchi)
Post a Comment