Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mjini hapa, tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Kegonga tarafa ya Ingwe wilayani Tarime mkoani Mara.
Imeelezwa kuwa miongoni mwa majeruhi ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Magamaga, Mohere Nyamhanga ( Chadema).
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, ugomvi wa mapanga ulizuka baada ya mabishano ya kisiasa kuibuka wakati watu hao walipokuwa wakijipatia vinywaji katika grosari ya Mwalimu Mwita Mohere.
Imeelezwa kuwa baadhi ya majeruhi wamelazwa katika vituo vya afya vya Mriba na Masanga.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii huku akiwa na jeraha la mgongoni, la kupigwa na kitu kizito, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Magamaga kupitia Chadema, Mohere Nyamhanga alisema wakati wakijipatia kinywaji kulizuka mabishano ya kisiasa yaliyoibua hisia kali.
Alisema alipojaribu kuzuia mtafaruku, alipigwa jiwe mgongoni na kuumia. Mwenyekiti huyo wa Kitongoji aliwataja wafuasi wa Chadema waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na yeye mwenyewe, Nyangi Chacha na Magasi Mwita.
Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi alitaja walioumia kwa kukatwa mapanga kuwa ni pamoja na Marwa Mohere, Nyamaretio Mwita na Pius Nyarengwa.
Baadhi yao watu hao wamelazwa wakiwa na majeraha makubwa katika vituo vya afya vya Mriba na Masanga.
Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Lazaro Mambosasa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaasa wanasiasa kuwa waangalifu na kuvumiliana.
“Jeshi letu linawaomba viongozi wa vyama vya siasa kutoa elimu kwa wafuasi wao kuendesha siasa kwa amani na bila kuingiliana na vyama vingine”, alisema Kamanda Mambosasa.
Post a Comment