Mbowe alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika jijini Mwanza, ambapo pia aliwatambulisha wabunge waliohamia Chadema kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge wa Kahama, James Lembeli na mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mara, Ester Bulaya.
Mbowe alisema viongozi wanaounda Ukawa, wanaendelea kushirikiana ingawa kuna changamoto kadhaa. Lakini, watatumia kila mbinu kuhakikisha anapatikana mgombea mmoja kwa ajili ya kupeperusha bendera ya Ukawa katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
“Tunaendelea kushirikiana lakini kuna changamoto, kama viongozi tutatumia kila mbinu tuwe na mgombea mmoja wa Ukawa na mazungumzo yoyote yanahitaji uvumilivu, kuheshimiana na kushirikiana,” alisema Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai.
Hata hivyo, Mbowe alisema umoja huo hautatangaza mgombea wao kwa haraka, kama ambavyo wananchi wanatarajia, kwa sababu tu CCM wamekwisha kumtangaza wao, ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
“Tutamtangaza mgombea wetu kwa muda muafaka na watanzania wote watafurahi…hatuwezi kutangaza kwa sababu tu CCM wametangaza mgombea wao,” alisema Mbowe.
Post a Comment