Na ingawa Sugu alidai bungeni pia kuwa hulipa ada ya sh. milioni tatu kwa mwaka kwa ajili ya elimu ya mtoto huyo, Faiza amedai ni kwa nusu ya pili tu ya kipindi cha miaka miwili ambayo amekuwa akisoma.
Aidha, mwanamitindo Faiza amesema hayupo tayari kumaliza kifamilia mvutano wa malezi ya mtoto na 'Sugu', kama Mbunge huyo alivyoeleza bungeni juzi.
Akizungumza katika chumba cha habari cha Nipashe jijini jana, Faiza alisema 'Sugu', mwanamuziki wa hip hop pia, hutoa sh.500,000 za matumizi ya mtoto lakini si kila mwezi.
"Bahati nzuri fedha hizi huwa anazituma kwa njia ya simu, kuna rekodi ya miamala (itathibitisha)... hatumi kila tarehe moja kwa mfano," alisema.
"Katika miezi sita iliyopita? Katika miezi sita iliyopita ametuma si zaidi ya mara nne."
Faiza alisema Mbunge wa Mbeya Mjini huyo alianza kulipa ada ya shule hivi karibuni, lakini mtoto huyo wa miaka miwili na miezi nane alianza kusoma akiwa na mwaka mmoja na miezi saba.
Kuhusu nia ya Sugu ya maridhino, Faiza alisema "haya mambo hayataisha kifamilia.
"Kama angekuwa anataka suluhu ya kifamilia kama alivyodai bungeni, wazazi wangu anawajua. Wazazi wake na ndugu zake wote nawajua, hakuwahusisha akakimbilia mahakamani.
"Siwezi. Acha haya mambo tukaamuliwe na mahakama (ili) haki itendeke."
Faiza anakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Mwanzo Manzese kumpa 'Sugu' haki ya kuishi na mtoto.
Mahakama ilimpa 'Sugu' haki hiyo baada ya Mbunge huyo kuonyesha hofu ya mtoto kukosa malezi mema kutoka kwa mama yake kutokana na mapenzi ya Faiza katika mavazi mafupi, ikiwemo pedi za wagonjwa au wazee, na nguo ziachazo wazi sehemu kubwa ya mwili.
Faiza amesema ingawa Sugu anamtuhumu kukosa maadili kwa sababu ya mavazi mbunge huyo amewahi kutolewa kwa nguvu bungeni na kurekodi CD zenye matusi za 'Anti Virus', vitendo ambavyo ni picha mbaya kwa mtoto siku za usoni.
Faiza alikutana na Sugu kupitia mtandao wa kijamii wa 'facebook' 2011 na aliondoka nyumbani kwa Mbunge huyo "baada ya kushindwa"; Januari mwaka jana, alisema.
Nipashe,28/06/2015
Post a Comment