Mbio za urais ndani ya CCM sasa zimefikia pabaya baada ya kuibuka hofu ya kuwapo kwa mpango wa kuivuruga Kamati Kuu kabla ya haijakutana kuchuja majina ya makada watakaotakiwa kupigiwa kura na Halmashuri Kuu ili kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu.
Hadi sasa CCM haijatangaza ratiba yake kwa ajili
ya kuongoza wanachama wanaotaka kuwania uongozi wa ngazi mbalimbali kwa
tiketi ya chama hicho.
Hata hivyo, Mwananchi ilitaarifiwa wiki hii kuwa
Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20 na kufuatiwa na vikao vya siku mbili
vya Halmashauri Kuu Mei 21 na 22 kwa ajili ya kupitisha ratiba, ilani na
taratibu nyingine za uchaguzi, ikiwa ni kuashiria kuanza rasmi kwa
mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho kikongwe.
Wakati chama kikitafakari kuanzisha rasmi mchakato
wa uchaguzi, tayari kuna habari kuwa moja ya makundi ya makada
wanaowania urais limeonyesha kutokuwa na imani na mwenendo wa Kamati Kuu
ambayo ina jukumu la kuchuja wanaowania urais na kupeleka majina
Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
Taarifa ambazo Mwananchi limezipata zinaeleza
kuwa kundi hilo linashawishi wanachama ili wakubali kuomba kupiga kura
ya kutokuwa na imani na Kamati Kuu kwa madai kuwa inaonekana kupendelea
baadhi ya waliojitokeza na kubana wagombea wengine.
Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa kundi hilo
limekuwa likifanya vikao mbalimbali vya kuweka mkakati wa jinsi gani ya
kuivuruga Kamati Kuu kabla ya kuchuja majina ya wagombea urais kwa
tiketi ya CCM.
“Kuna mkakati wa kuweka CC itakayowasaidia kwa
kuwa ukishapita hapo, umeshakuwa Rais wa nchi hii. Uzuri ukishinda ndani
ya chama na kutangazwa kuwa mgombea wao, basi makundi yote hurudi
kukipigania chama na wengine kujipendekeza ili wapewe nafasi katika
serikali ijayo,” alisema mpashaji habari wetu ambaye ni mmoja wa
viongozi wa juu wa CCM.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mpango huo unafanyika
kwa umakini mkubwa ili kuweza kuhakikisha Kamati Kuu haikati jina la
mgombea wa kundi hilo kama ambavyo imewahi kufanyika kwa makada wengine
ambao majina yao hayakupelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya
kupigiwa kura kutokana na nguvu yao kwenye chama.
Kama hilo litafanikiwa itakuwa ni kwa mara ya pili
kutokea baada ya mwaka 1995, Jakaya Kikwete kumlalamikia aliyekuwa
katibu mkuu wa CCM, Lawrance Gama kuwa hawezi kumtendea haki baada ya
kuonekana akiwa amevaa nguo yenye nembo ya mmoja wa waliokuwa wakiwania
kuteuliwa na chama hicho kugombea urais.
Alipoulizwa kuhusu mkakati huo, katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kuwa wamesikia na kuelezwa kuwa
kundi hilo linagawa fedha kufanikisha jambo hilo kwa kuwa wanadhani
sekretarieti ya chama haiwapendelei wao.
“Wanadhani kuna watu wanapendelewa, kama suala
hilo lipo bila shaka chama hakiwezi kukaa kimya kwani huo ni uasi na
usaliti kwa chama,” alisema Nape.
Alisema kuwa ndani ya chama viko vyombo vingi ambavyo kama mtu ana shida anaingia kwenye mikutano sahihi ya chama.
“Mtu huwezi kutengeneza vikao nje ya vikao halali halafu urudi kuongoza chama hicho hicho,” alisema Nape.
“Labda watu wana mpango wa kukivuruga chama hiki
halafu wagombee kwa chama kingine sawa, lakini kama wanataka kugombea
humuhumu CCM, haitawezekana,” alisema Nape.
Mmoja wa wajumbe wa CC ambaye pia ni Meya wa
Ilala, Jerry Silaa alipoulizwa kuhusu mkakati huo kama amesikia, hakuwa
tayari kusema chochote kwa kuwa yeye yupo ndani ya Kamati Kuu.
Hadi sasa makada sita wa CCM wamefungiwa kwa zaidi
ya miezi 12 kujishirikisha na harakati za uchaguzi ndani ya chama.
Makada hao ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick
Sumaye.
Pia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Pia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Baadhi ya makada wanaotajwa kutaka urais kwa
tiketi ya chama hicho ni pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, waziri wa
zamani wa Ulinzi, Emmanuel Nchimbi, waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani,
Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na Waziri wa
Ujenzi, John Pombe Magufuli.
Alipoulizwa kama kuna watu wanapita kushawishi
wanachama kujiunga na mkakati huo, mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa
Shinyanga, Khamis Mgeja alisema hofu hiyo inatokana na chama kuchelewa
kuruhusu wanachama wake kuingia kwenye mchakato.
“Kama chama kingeruhusu mapema, kingedhibiti mapema mambo haya,” alisema Mgeja.
Muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo, Mgeja,
ambaye anaingia kwenye vikao vya Halmashauri Kuu ya CCM kutokana na
nafasi yake kwenye mkoa, alipiga simu na kumweleza mwandishi kuwa
anataka kuwatoa hofu wanachama wa CCM kuwa chama kiko imara na hakuna
ajenda ya mpasuko ndani ya chama.
Akizungumza na gazeti la Mwananchi kwa simu, Makamba,
ambaye ni mbunge wa Bumburi, alisema amesikia kuwapo kwa mpango huo
lakini hajathibitisha.
“Hata mimi nimezisikia habari hizo ingawa
hazijathibitishwa. Kwa kuwa hazijathibitishwa, siwezi kuzungumzia
kiundani,” alisema Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi na
Teknolojia.
“Nachoweza kusema ni kwamba chama chetu kina
utaratibu, kinatabirika na kinaeleweka. Hakuna haja ya kuwa na papara
katika hili na mimi sina hofu na hili kwa kuwa najua kila kitu
kitakwenda kama ilivyopangwa.”
Alisema anajua kuwa uteuzi utafanyika miezi miwili
kabla ya uchaguzi ili utakapofika mwezi Agosti chama kipeleke majina
kwenye Tume ya Uchaguzi yakiwa yamechujwa kwa umakini bila ya kuwa na
papara ya aina yoyote.
Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambao wote wanatajwa
kuwamo kwenye mbio za urais, hawakutaka kuzungumzia suala hilo, Membe
akisema yuko safarini kikazi na Sumaye akisema hajasikia habari hizo.
Juhudi za kumpata Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa hazikufanikiwa.
Credit: Mwananchi
Credit: Mwananchi
Post a Comment