RAIS
wa Burundi, Pierre Nkurunziza, amewekwa mtegoni baada ya Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Jakaya Kikwete, kuitisha mkutano
wa wakuu wa nchi hizo.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka Makao Makuu ya EAC jijini Arusha, kikao hicho
cha dharula kinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Jumapili hii.
Huu
unachokuliwa kama mtego kwa Nkurunziza ambaye wakati wa kikao kingine
kama hicho kilichofanyika Mei 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam,
wanajeshi nchini humo, chini ya shushushu namba moja wa zamani wa nchi
hiyo, Meja Jenerali Godfroid Niyombare, walifanya jaribio la kupindua
serikali yake.
Pamoja
na Rais Nkurunziza na Kikwete, kikao cha wakuu wa nchi za EAC
hujumuisha pia marais Paul Kagame (Rwanda), Yoweri Museveni (Uganda) na
Uhuru Kenyatta wa Kenya, ingawa pia viongozi wa nchi nyingine wanaweza
kualikwa hasa katika suala kama hili la mzozo nchini Burundi.
Nkurunziza
alilazimika kukaa mafichoni jijini Dar es Salaam hadi baada ya
wanajeshi wanaomtii kujibu mashambulizi na kumaliza mapinduzi hayo.
Tangu
wakati huo, kumekuwa na maandamano na vurugu nchini Burundi kupinga
mpango wa Nkurunziza kugombea muhula wa tatu wa urais, huku vifo kadhaa
vikiripotiwa.
Na
sasa, wakuu wa nchi hizo wanatazamiwa kukutana tena Jumapili hii kwa
mzunguko wa pili wa mazungumzo ya kutafuta utatuzi wa mzozo huo.
Wito
wa Kikwete kwa Nkurunziza unachukuliwa kama mtego na kuna kila dalili
kuwa huenda asihudhurie ingawa kukosekana kwake kutapunguza ushawishi
ambao angeweza kuufanya kwa viongozi wenzake ambao miongoni mwao, kama
Uhuru wa Kenya, wanakosoa uamuzi wake wa kugombea muhula wa tatu.
Taarifa
katika mitandao kadhaa zilimnukuu msemaji wake, Gervais Abayeho,
akisema nchi hiyo itatuma wawakilishi; “kwa sasa ni mapema kufahamu ni
akina nani watakaoiwakilisha Burundi.”
Mbali
na Rais Uhuru Kenyatta, viongozi kadhaa wa Afrika walimshauri
Nkurunziza kuheshimu matakwa ya raia wake huku Rais Thabo Mbeki wa
Afrika Kusini akisema: “Nkurunziza asipoachana na mpango wake huo,
atalilirudisha taifa lake kwenye vita.”
Wabunge wa EALA wazamia Arusha
Wakati
Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EALA) ikijiandaa kutembelea Burundi kujionea madhara yaliyosababishwa
na mzozo unaoendelea, kuna taarifa kuwa wabunge kadhaa wa Bunge hilo
kutoka Burundi bado wapo jijini Arusha.
Uchunguzi
wetu umebaini kuwa wabunge watatu au wanne kati ya tisa waliokuwa
wakishiriki kikao cha EALA wanaendelea kuishi nchini.
Akizungumza
kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wabunge hao alisema wameshindwa
kurejea nyumbani kutokana na hali mbaya ya usalama iliyopo huko.
“Tumekuwa tukiwasiliana na wenzetu Burundi na wametuambia si salama sana kwa sasa kurejea huko, ndio maana bado tupo hapa,” alisema Mbunge huyo.
Wiki iliyopita EALA ilimaliza kikao cha wiki mbili jijini Arusha na wabunge kutoka mataifa mengine waliondoka Jumamosi.
Mbunge huyo hakuwa tayari kueleza ni nani anawalipia gharama za hotelini kwa sasa na kwa muda gani wataishi nchini.
Wabunge
tisa wanaoiwakilisha Burundi EALA ni Emerence Bucumi, Hafsa Mossi,
Isabelle Ndahayo, Leonce Ndarubagiye, Martin Nduwimana, Emmanuel Nengo,
Jeremie Ngendakumana, Frederic Ngenzebuhoro na Yves Nsabimana.
>>Raia Tanzania.
Post a Comment