WABUNGE
wameishauri serikali kulipa deni la makandarasi wanaoidai Wizara ya
Ujenzi linalozidi Sh. bilioni 850 kuwezesha bajeti iliyotengwa kufanya
kazi za maendeleo.
Hayo yalitokea jana bungeni mjini Dodoma wakati wabunge hao wakichangia bajeti ya wizara hiyo ya takriban Sh. bilioni 900.
Akisoma
hatuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Muhambwe, Felix
Mkosamali (NCCR Mageuzi), alisema fedha iliyotengwa kwa ajili ya
maendeleo katika wizara hiyo ni ndogo.
Alisema
ujenzi ni sekta ambayo kibajeti inachukua asilimia kubwa, lakini
kiuhalisia ina madeni makubwa kutoka kwa makandarasi na washauri.
“Waziri
wa Fedha, Saada Mkuya, alisema kipo kikosi kazi cha kuhakiki madeni ya
wazabuni kwa wizara mbalimbali. Moja ya wizara hizo ni hii ya ujenzi.
“Kambi
Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, kueleza
kikosi kazi kilichoundwa kuhakiki uhalali wa madeni ya wizara kimebaini
ni kiasi gani kinachodaiwa,” alisema Mkosamali.
Alisema
wizara hiyo hadi sasa inadaiwa Sh. biloni 800 na hakuna majibu ya namna
yatakavyolipwa pamoja na mbwembwe za uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara
ya Ujenzi.
“Pamoja na kelele na mbwembwe nyingi, ukweli ni kwamba madeni ya wizara yanazidi fedha za maendeleo tunazopitisha bungeni,” alisema.
Alisema mwaka 2014/2015, madeni ya wizara hiyo yalikuwa Sh. bilioni 760 huku bajeti ya maendeleo ikiwa ni Sh. bilioni 762.
“Ni
dhahiri kuwa wizara haikuwa na fedha za maendeleo kwa mwaka huo wa
fedha. Hivyo waziri alieleze ukweli Bunge kwenye Bajeti hiyo ni fedha
kiasi gani zimelipa madeni?” alihoji.
Mkosamali
alisema zipo taarifa kwamba makandarasi watatu wamekufa kutokana na
msongo wa mawazo baada ya serikali kutowalipa madeni yao walipomaliza
kazi.
Akizungumzia
ununuzi wa kivuko cha Bagamoyo, Mkosamali alisema kilinunuliwa kwa
shilingi bilioni nane, kinabeba abiria 300 huku kikitumia saa tatu
kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo.
“Ni
jambo la ajabu kununua kivuko cha kizamani, chakavu chenye spidi ndogo.
Bakhresa ana meli inayotoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa dakika 90
tu ikiwa na abiria 500 na taarifa tulizonazo, bei yake ni kati ya Sh.
bilioni 4 na 5 tu.
“Tunaomba
Bunge kuunda Tume itakayochunguza ununuzi wa kivuko hiki kibovu na cha
kizamani kilichonunuliwa kwa bei kubwa huku kikienda mara moja tu
Bagamoyo kwa siku,” alisema Mkosamali.
Mbunge
wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema serikali imeshindwa
kutatua kero ya foleni jijini Dar es Salaam pamoja na majiji mengine
makubwa na kwamba juhudi za makusudi zinapaswa kufanyika kunusuru
wananchi wa miji hiyo.
Awali
akiwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo, Dk. Magufuli alisema fedha
walizoomba ni zaidi ya Sh. bilioni 900 zitakazosaidia maendeleo ya
kuboresha barabara, madaraja na vivuko katika maeneo mbalimbali.
Post a Comment