Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, wamesema hawapo tayari
kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kwa kitendo cha
kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema.
Wametoa tamko hilo jana mbele ya waandishi wa habari katika ofisi kuu za CCM Kisiwandui.
Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya wanachama wezake, Katibu
wa mkoa wa mjini CCM, Muhammed Nyawenga, alisema Lowassa asidhani kuwa
wanachama wengi wa CCM walimuunga mkono wakati alipotangaza nia ya
kugombea urais wa Muungano kupitia chama hicho, akadhani kuwa na sasa
watakuwa pamoja naye.
Alisema wanachama wa CCM hususan kutoka Zanzibar
wanachoangalia kwanza ni chama na mtu baadae hivyo kama kaamua kujiunga
Chadema hawako pamoja naye.
“Tunamwambia Lowassa kama mvuvi wa pweza basi tutakutana mwambani,”alisema kupitia tamko hilo.
Walisema wanashangazwa na baadhi ya vyama vya upinzani hasa
vile vinavyouunda Ukawa namna wanavyoendelea kuendesha siasa za
ubabaishaji na ulaghai kwa Watanzania.
Alisema ni jambo la aibu na la kufedhehesha kuona kwamba
hata baada kufikisha umri wa miaka 23 tangu kuanzishwa rasmi kwa vyama
vya upinzani bado vyama hivyo vimeshindwa kuandaa wagombea wenye uwezo
wa kuwaongoza Watanzania na kuishia kudaka mapumba yanayotoka CCM.
Alisema uamuzi wa Lowassa kutoka CCM sio jambo la kukishtua
chama, wanachama wala viongozi wa chama hicho na kamwe CCM haiwezi
kudhoofika wala kupasuka kwani sio mara ya kwanza kwa CCM kuondokewa na
kiongozi muandamizi na kujiunga na upinzani.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa mjini Magharibi ambae alikuwa
kinara katika kumuunga mkono Lowassa wakati akiomba ridhaa ya chama
hicho kugombea urais kupitia CCM, Borafya Silima Juma, alisema kiongozi
huyo anapenda madaraka na ukubwa na ndio maana baada ya jina lake
kutopita ameamua kujiunga na Chadema.

Post a Comment