MTU mmoja ambaye ni mkimbizi kutoka
Burundi, amefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wenye dalili
zinazofanana na Ugonjwa wa Ebola katika Kambi ya Nyarugusu mkoani
Kigoma.

Marehemu huyo aliyejulikana kwa jina la
Buchimu Joel, alifariki dunia jana Agosti 10, 2015 katika Hospitali ya
Mkoa wa Kigoma ya Maweni, baada ya kuugua kwa siku kadhaa akiwa katika
Kambi hiyo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo,
Shija Ganai, amekaririwa na FikraPevu akisema kwamba mtu huyo alikuwa
akitokwa na damu katika sehemu zote za matundu za mwili wake na kwamba
sampuli za damu na vitu vingine zimepelekwa Jijini Dar es Salaam kwa
uchunguzi zaidi.
Aidha, amebainisha kwamba kutokana na
dalili hizo ambazo zinafanana na za ugonjwa wa Ebola, wataalamu wa afya
walimhudumia kwa kufuata misingi ya kutibu magonjwa ya Ebola ambapo
wamelazimika kumzika kwa kufuata taratibu pamoja na kuweka tahadhari
katika Karantini ya maeneo aliyokaa akiwa mgonjwa pamoja na ndugu wa
karibu.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, homa ya
Ebola ilianza nchini Guinea na kutapakaa nchi jirani za Sierra Leone na
Liberia mwaka jana huku ikielezwa kuua watu wengi ambao idadi yao hadi
sasa inadaiwa kuzidi watu 10,000 baada ya kuibuka kwa tishio la ugonjwa
huo katika siku za karibuni katika mataifa mbalimbali mapema mwaka huu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii, dalili za awali za ugonjwa huo ni homa kali ya ghafla, kulegea
mwili, maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda
kooni.
Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na
kutapika, kuharisha, kutokwa na vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa
kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa, hutokwa damu ndani na nje ya
mwili.
Serikali ilisema katika mkoa wa Dar es
Salaam, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Temeke Isolation Unit,
zilitengwa maalum kwa kuhudumia wagonjwa wa ebola endapo watatambuliwa
ambapo eneo la Temeke linaelezwa kuwa limeboreshwa kwa kuzingatia vigezo
maalumu ili likidhi mahitaji ya matibabu ya ugonjwa huu.
Post a Comment