MKURUGENZI
wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amewaunga mkono wanachama
na makada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wanaohamia vyama vya upinzani.
Alisema makada hao walichelewa kutoka ndani ya chama hicho na wameondoka wakati tayari chama hicho kimeharibika.
Butiku aliyasema hayo alipotoa mada kwenye mdahalo wa Maadili na Haki kuelekea Uchaguzi Mkuu, Dar es Salaam jana.
Alisema CCM ni sawa na kokoro ambalo limebeba kila aina ya uchafu.
Butiku
alisema hakubaliani na makada wanaoondoka ndani ya CCM hivi sasa kwa
hoja ya kunukuu kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba wanakwenda
nje ya CCM kutafuta mabadiliko.
“Sikubaliani
na wanaoondoka sasa ndani ya CCM wakati wakijua fika wamekwisha
kukiharibu chama tangu mwaka 1995 baada ya watu 10 kuasisi kundi
lililojulikana kama Mtandao.
“Kama
wangeondoka wakati Nyerere alipotoa tamko hilo ningewaunga mkono,
lakini wao wameendelea kukiharibu chama wakitumia mizengwe na hawataki
utaratibu.
“Profesa
Baregu (Mwesiga) wapokee ni safi, wapokeeni, waungwana wanapoona
hawakubalini na misimamo ya mtu huwa hawavurugi ila hutoka mara moja na
si kuchafua nyumba ya watu ndipo unatoka. Mangula mmewavumilia sana kwa
misimamo yao,” alisema.
Butiku
pia alitumia mdahalo huo kuzungumzia hoja ya utajiri wa viongozi
akisema usitumiwe kukandamiza wanyonge na kwamba suala la mtu kuwa
tajiri siyo tatizo bali ni kutazama utajiri wake unatumikaje.
“Sitaki kukubalina na wale wanotumia utajiri kwa kuwatupia watoto fedha chini na kuumizana wakinyang’ anyana,” alisema.
Alisema
taasisi yake itaendelea kukosoa kama wanavyofanya kwa CCM ilipokuwa
ikikosea ndivyo itakavyofanya kwa Ukawa kwa kuwakataa.
Butiku
alitoa siri iliyomfanya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kulikataa kundi
la mtandao mwaka 1995 kwamba ni Rais Mwinyi ambaye aliwashtaki kwake
kuwa ni kundi linalotumia fedha kutafuta uongozi.
Profesa Baregu amtetea Lowassa
Mjumbe
wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu
alisema Chadema kimekubali kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kwa sababu Serikali ilishindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake
kuwa anahusika na Kampuni ya Ufuaji umeme ya Kampuni ya Richmond.
“Vikao
vingi vya chama vimekaa kuchambua na kutafakari kuhusu mahali ambako
panaonyesha Lowassa kahusika na tuhuma za ufisadi wa Richmond.
“Hatukuweza
kubaini hilo ndiyo maana hata hapa tulipo, awe mimi au mtu mwingine
hawezi kueleza moja kwa moja kuhusiana na suala la Richmond,” alisema Profesa Baregu.
Kuhusu
maadili, Profesa Baregu alisemaTume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imejikuta ikishindwa kuaminika na wananchi kutokana na kutoweka wazi
mfumo wa uhakika wa uandikishaji kwa mfumo wa elekroniki (BVR).
Awali
msomi huyo alilimwagia sifa Jeshi la Polisi kwa kuonyesha ukomavu kwa
kulinda maandamano ya mgombea wa Chadema-Ukawa kwenda NEC kuchukua fomu
ya kugombea urais, Edward Lowassa, kwa amani bila bughudha.
Polepole
Naye
Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole
alisema alipokua akizungumza kwenye mijadala iliyopita kuhusu mchakato
wa upatikanaji wa Katiba Mpya kwamba ulikua unaharibiwa na baadhi ya
wanasiasa wa CCM ambao walikua na maslahi binafsi alikua akipigiwa
makofi, jambo ambalo anaamini walikuwa hawajamuelewa.
Alisema kuna wakati alibadilika jambo ambalo lilisababisha viongozi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutomuelewa pia.
“Kuna
wakati nilisimama na kuzungumzia ukweli lakini baadhi ya watu
hawajanielewa lakini nilikua na malengo kuwa baadhi ya watu wanaipinga
Katiba kwa maslahi yao binafsi.
“Wakati
wa mchakato wa Katiba tulitukanwa tulidhalilishwa na kuzomewa, hii
inatokana na kupiga kelele za kuwaambia wananchi kuna watu ndani ya CCM
wanavuruga mchakato huu kwa maslahi yao binafsi,” alisema Polepole.
Alisema
alipokua CCM aliwaambia wananchi kuwa CCM imekosea na Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) walimuunga mkono, lakini hivi sasa Ukawa
wanapokosolewa wanakasirika.
“Nilipokua naisema CCM Ukawa walifurahi lakini hivi sasa naisema Ukawa wanakasirika kwa sababu gani hawapendi kukosolewa,” alihoji.
Jaji Manento
Jaji
Mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Amir Manento,
alisema NEC inapaswa kutenda haki ili kuendeleza amani nchini.
Alisema
katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, NEC ilikuwa na jukumu
la kuwaandikisha wapiga kura lakini baadhi yao wamedai majina
hayajaonekana katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“NEC
inapaswa kuwa ‘Apex’ nikimaanisha ni juu kabisa wasiweze kuwabeba watu
wengine hali ambayo inaweza kuhatarisha amani ya nchi,” alisema Jaji Manento.
Alisema
wakati wa kupiga kura matokeo yanapaswa kuwasilishwa kuanzia ngazi ya
wilaya na kupelekwa makao makuu ya Tume jambo ambalo linasababisha
kuwapo vitendo vya uchakachuaji.
Aliwataka kutenda haki kuepusha vurugu zinazoweza kujitokeza.
Mangula
Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alisema chama hicho kina kanuni na
maadili ya uongozi na anayebainika amezikiuka anachukuliwa hatua.
Alisema kama ambavyo CCM imekuwa ikihakikisha kanuni zake zinasambazwa ndivyo ambavyo NEC inatakiwa kufanya kazi zake.
~Mpekuzi blog
Post a Comment