Mwanza/Dar. Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake kimeshindwa kumtangaza
mgombea wake wa urais kama ilivyotarajiwa jana, badala yake kikawaomba
Watanzania kutokuwa na haraka, wasiwasi wala mihemko na kuwa muda
ukifika kitamtangaza.
Akihutubia mkutano wa hadhara
katika Viwanja vya Magomeni jijini hapa, Mbowe aliwaomba wananchi
kuuvumilia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa sababu viongozi wake
wanaendelea na majadiliano na watakapokubaliana watamtangaza mgombea
wao.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar),
Salum Mwalimu alisema ilikuwa wamtangaze mgombea urais kama
ilivyoripotiwa na gazeti hili, lakini wenzao wa CUF wamewaomba kuwa
wanaendelea na vikao vyao vya chama.
Naibu Katibu Mkuu
wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema: “Wengi wana hamu ya kutaka kujua
mgombea urais wa Chadema, naomba niseme kwamba tumekuja Mwanza kwa
mambo mawili, kuja kuwapokea makamanda hawa wawili na kuitokomeza CCM.
“Ukawa
itamsimamisha mgombea urais ambaye Oktoba lazima aiondoe CCM
madarakani, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Magdalena Sakaya) ametuomba tena
tusubiri hadi tarehe 25 (Jumamosi), kwani watakuwa na kikao cha Baraza
Kuu la chama hicho, hivyo tunawasubiri wenzetu.”
Mbowe
aliyetumia mkutano huo kuwakabidhi kadi wanachama wapya waliotoka CCM na
kujiunga Chadema, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Mbunge wa Viti
Maalumu, Ester Bulaya, aliweka msisitizo:
“Muungano
wetu wa Ukawa ni wa msingi sana, kuna changamoto, tunaomba wananchi muwe
wavumilivu, tuache mihemko ili tufikie uamuzi sahihi.
“Tunaomba
mtuvumilie, hatuwezi kumtangaza mgombea wetu kwa sababu tu CCM
wametangaza wa kwao, hapana! Tutamtangaza mgombea wetu na nyote
mtafurahi,” alisema Mbowe huku akishangaliwa na maelfu ya wananchi.
Alisema,
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikuwa ahudhurie mkutano huo
lakini kutokana na foleni za Dar es Salaam alishindwa kuwahi ndege na
kwamba, viongozi wengine wa CUF na NCCR Mageuzi walialikwa lakini
walikuwa na vikao vya vyama vyao.
Mbowe alisema Ukawa
ni mpango wa wananchi, siyo wa viongozi na kwamba ulianzishwa Dodoma na
viongozi wote wa upinzani na Kundi la Wabunge 201 wa Bunge Maalumu la
Katiba walihudhuria, lakini baadhi yao walipenyezewa ‘kitu kidogo’
wakaondoka hivyo kubaki vyama vinne vya siasa.
Udini, ukabila wamkera
Mbowe
alionyesha kusikitishwa na kauli alizodai kutolewa na viongozi wa CCM,
kumnadi mgombea wao kwa ukabila na kuwataka wananchi kuwakataa
wanaotumia mbinu hizo kwani hali hiyo inaweza kusababisha machafuko.
“Nafurahishwa
sana na kauli zinazotolewa na viongozi wa CCM, tunampata kiongozi kwa
ukabila! Ukawa hatutamchagua mgombea wetu kwa misingi ya ukabila wala
udini, huo ni upumbavu,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Msikubali
kurudisha ukabila wala udini, hapa uwanjani tupo makabila mengi,
Wasukuma mpo! Wahaya, Wachaga, (Ezekiel) Wenje (Mbunge wa Nyamagana) ni
Mjaluo yupo hapa.”
Alisema Watanzania wanataka mabadiliko na kwamba hali hiyo imeshuhudiwa wakati wa uandikishaji wa daftari la wapigakura.
Aonya wizi wa kura
Mbowe
alisema hawatakuwa na tatizo iwapo ushindi utapatikana kwa njia za
haki, lakini hawatakuwa na suluhu iwapo utatumika wizi wa kura
kumuingiza mgombea madarakani.
“Hatutapiga magoti na
kuomba, kama ushindi utapatikana kwa njia halali hatuna tatizo, lakini
tukiona mambo yanakwenda ndivyo sivyo tunasema polisi mtatusamehe,
mabomu hayatatosha,” alisema Mbowe.
Lembeli, Bulaya waombewa msamaha
Mbowe alisema Chadema kina maadili yake na kwamba Lembeli na Bulaya waliokuwa CCM wametenda mengi lakini anawaombea msamaha.
“Naomba muwasamehe. Wangapi wanasema tuwasamehe?” alihoji Mbowe huku akiitikiwa kwa sauti, “Woteee”.
Alisema viongozi hao ni miongoni mwa wengi wanaokaribia kutimka CCM na kuwapongeza kwa ujasiri wao makini walioonyesha.
Aahidi kutaifisha viwanja vya CCM
Baada
ya kueleza jinsi alivyompigia simu bila mafanikio Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo kuomba kutumia Uwanja wa CCM Kirumba kwa
ajili ya mkutano huo, Mbowe alisema Serikali ya Ukawa ikiingia
madarakani itahakikisha viwanja vyote vilivyojengwa na wananchi
vinavyohodhiwa na CCM vinarejeshwa kwenye halmashauri.
“Chadema
kwa kushirikiana na Ukawa, viwanja vyote vilivyojengwa na wananchi
vitarejeshwa kwenye halmashauri ili vitumiwe na wananchi wote,” alisema
baada ya baadhi ya wanawake kuzidiwa na kuanguka kutokana na wingi wa
watu na ufinyu wa uwanja wa Magomeni.
Wagombea kulishwa yamini
Katibu
Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa aliwata wagombea ubunge
waliopitishwa ambao wana mawazo ya kuuza nafasi zao kwa CCM kujiengua
mapema kabla chama hakijawachukulia hatua.
Pia, Dk Slaa
alisema chama hicho kitatoa fomu maalumu ambazo zitasainiwa na wagombea
ubunge mahakamani ili kiweze kuwachukulia hatua za kinidhamu
watakaokwenda kinyume na taratibu za chama hicho.
“Majimbo
157 yamekamilisha leo (jana), sisi Chadema hakuna jimbo ambalo mgombea
atapita bila kupingwa kama wanavyofikiri CCM,” alisema Dk Slaa na
kuongeza:
“Tutatoa fomu za uteuzi ambazo wote
waliopitishwa kugombea ubunge watasainishwa mahakamani, naomba niseme
atakayeuza jimbo atashughulikiwa, kama mtu anataka kujitoa ajitoe
mapema.”
Dk Slaa alisema miaka 10 iliyopita wananchi
waliahidiwa maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini yamegeuka na kuwa
kinyume, sasa ni maisha magumu kwa kila Mtanzania.
“Waswahili
wanasema ukiumwa na nyoka hata jani likikugusa unakimbia, miaka 10
mliahidiwa maisha bora kwa kila Mtanzania, leo ni maisha magumu kwa kila
Mtanzania. Cha kwanza tunachokisimamia Chadema ni kurudisha nchi kwa
wananchi, CCM wamepoka madaraka ya wananchi na kuyaweka mikononi mwa
wachache, tunawaambia mwisho wao ni Oktoba,” alisema Dk Slaa.
Lembeli afunguka
Akizungumza
kwenye mkutano huo, Lembeli alisema: “Nakumbuka tarehe 16 nilisali
nikiwa kijijini kwetu na mama yangu mzazi, nikamwomba Mungu anitoe nchi
ya laana anipeleke nchi ya matumaini.
Tarehe 17 nikafanya uamuzi, sasa nipo uwanjani, naomba niwaambie sijaja Mwanza hivihivi nimekamilika, nilipotoka nimeaga.”
Lembeli aliongeza: “Nimezoea kusema msemo wangu huu, hebu kunja ngumi... koroga... peoples,” umati wa watu uliitikia “Power”.
Kabla
hajahutubia, Lembeli alibisha hodi Mwanza kwa kusema: “Hodi…hodi,
aliitikiwa kwa sauti na umati uliohudhuria: “Karibu baba, karibu.”
Bulaya ampa salamu Wasira
Akihutubia
baada ya kukabidhiwa kadi ya uanachama, Buyala alianza kwa kuwauliza
wananchi: “Nikamtoe? Nauliza, nikamtoe? Nikamtoe nani?” wananchi
walijibu kwa sauti kubwa: “Wasira... kamtoe Wasira.”
Bulaya
alisema ni bora kama Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Stephen
Wasira anamsikia akaondoka kama alivyomshauri Makongoro Nyerere.
“Makongoro
Nyerere alisema, awamu ya kwanza upo, awamu ya pili upo, ya tatu upo ya
nne upo ya tano mwisho wake umefika sasa,” alisema Bulaya.
Alisema
kwa Mkoa wa Mara yupo mwenyekiti wake, Vicent Nyerere ambaye atafanya
naye kazi kwa karibu na kwamba yeye na wenzake wa Chadema ni muziki
mnene na jeshi kubwa.
Lissu na kabila la CCM
Akihutubia
kwenye mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
aliwalinganisha, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Andrew Chenge
na Spika Anne Makinda kwamba hawana tofauti na mgombea urais wa CCM, Dk
John Magufuli, kwa sababu wote ni kabila moja la CCM.
“Nimefanya
mikutano mingi, kila mahala nilipokwenda nilikuwa naambiwa Dk Magufuli
kabila lake ni Msukuma, wengine Msubi na wapo waliosema Mzinza, mimi
naomba niwaambie kwamba kabila moja la CCM ndilo la Dk Magufuli,”
alisema Lissu.
Alisema Dk Magufuli ndiye aliyeuza
nyumba za Serikali nchi nzima, kauli ambayo ilitiliwa mkazo na Makamu
Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari ambaye alisema watumishi
wa umma wanaishi kwenye nyumba za vichochoroni kutokana na Dk Magufuli
kuuza nyumba za Serikali.
Mwenyekiti wa Baraza la
Wadhamini wa Chadema, Arcado Ntagazwa ambaye aliwahi kuwa waziri na
naibu waziri kwa miaka 15 alisema: “Safari hii kwa Chadema na washirika
wao wa Ukawa ni moja kwa moja Ikulu.
Goli la mkono laibuka
Ntagazwa alisema: “Mambo ya kusema goli la mkono, watambue kwamba Oktoba ndiyo mwisho wa ufisadi,”
Kauli
hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye alisema mwaka
huu goli la mkono litawageukia wao... “Wakijifanya wao ni watoto wa
kihuni makamanda wa Chadema ni wahuni zaidi yao.”
Kuhusu kucheza rafu, Mwalimu alisema wanaotarajia kucheza rafu kwenye uchaguzi mkuu ni wazi kwamba wameshindwa kucheza uwanjani.
“CCM
kutangaza kushinda hata kwa goli la mkono ni wazi kwamba wameshindwa
kucheza uwanjani sasa sisi tutawafuata hukohuko nje ya uwanja na
tutawabana,” alisema Mwalimu.
Wenje, Kiwia watamba
Mbunge
wa Nyamagana, Ezekia Wenje na Highness Kiwia, walisema kwa sasa wapo
likizo ya miezi miwili na wanatarajia kuapishwa tena kuwa wabunge baada
ya uchaguzi.
Kiwia alisema: “Mimi ndiye rais wa Jamhuri
ya watu wa Ilemela, sina shaka tumemaliza kura za maoni sasa nasubiri
tena kuwa Mbunge wa Ilemela.”
Akihutubia, Nyerere
ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini, alisema kazi inaendelea na
kinachofanyika sasa ni kuhakikisha CCM inaondoka madarakani Oktoba.
Leo viongozi hao wa Chadema watakuwa na mkutano mwingine mjini Mbeya na baadaye Arusha na Jumatatu ni Dar es Salaam.
Imeandikwa na Midraji Ibrahim, Aidan Mhando na Fidelis Butahe
Post a Comment