Wanachama wa Chadema wamedai kufichua mpango unaofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM wa kumwekea pingamizi Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe ili asiwanie ubunge.
Kiini cha mipango
hiyo ni hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Hai iliyomtia hatiani kwa kosa
la kumshambulia mwangalizi wa ndani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010,
Nassir Yamin.
Katika hukumu hiyo, iliyotolewa Juni 17
na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Dennis Mpelembwa alimhukumu Mbowe
kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja.
Hata
hivyo, Mbowe ambaye ni mgombea pekee na kushinda kura za maoni kwa
kupata 269 za ndiyo na tano za hapana, alilipa faini hiyo na kuachiwa
huru baada ya wafuasi wake kuchanga fedha hizo.
Mipango
hiyo inayodaiwa kuwa ni ya CCM kutaka kutumia hukumu hiyo kumzuia Mbowe
kuwania ubunge, ilielezwa juzi katika Mkutano Mkuu maalumu wa kura za
maoni za ubunge Jimbo la Hai.
Mmoja wa wajumbe wa
mkutano huo, James Swai alimuuliza Mbowe amejiandaaje, kwa sababu kuna
madai kuwa CCM wana mpango wa kutumia kesi hiyo ili kumwengua kugombea
nafasi hiyo.
Hata hivyo, wakati akijibu swali hilo,
Mbowe hakueleza wazi kama anafahamu mpango huo zaidi ya kuitaka CCM
isitafute ushindi wa mezani.
“Wangekuwa na wanasheria
wasingefikiria kabisa wala kuzungumza hivyo. Kifungu nilichohukumiwa
nacho hakinizuii kugombea. Wasitafute ushindi wa mezani waje uwanjani,”
alisema Mbowe.
Mbowe alisema tayari jopo la mawakili
sita wa Chadema, ambao hata hivyo hakuwataja kwa majina, limeweka
mkakati maalumu wa kukata rufaa kupinga hukumu hiyo aliyodai ni batili.
Post a Comment