MCHEPUKO usitajwe kwako! Mrembo aliyejulikana kwa jina la Bahati Nyamkira (20) (pichani), mkazi wa Kijiji cha Singu, Kata ya Kukirango, Butiama, Mara, amenusurika kifo baada ya kucharangwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili na mwanaume anayedaiwa kuwa hawara yake kisa kikisemekana ni kumkuta akiwa na hawara mwingine, (kuwagonganisha).
Bahati Nyamkira amenusurika kifo baada ya kucharangwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili.
Tukio hilo la kushangaza lilitokea saa 4 usiku wa Mei 23, mwaka huu nyumbani kwa mwanamke huyo katika kijiji hicho.Kwa mujibu wa mashuhuda, siku ya tukio, saa 2 usiku, kijana mmoja aitwaye Nyamkinda James (23), mkazi wa Kijiji cha Buturu ambaye anadaiwa aliwahi kuishi na mwanamke huyo na kuzaa naye mtoto mmoja, alikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo kwa lengo la kumchukua ili aende kulala naye kwao lakini mwanamke aligoma na kumfanya mwanaume huyo kutia shaka kwamba, huenda ana mwanaume mwingine.
Ilizidi kudaiwa kuwa, mara baada ya mwanamke huyo kugoma, kijana huyo aliondoka kimyakimya hadi nyumbani kwao na kuchukua panga kisha akarudi kwa kunyatia na kujificha sehemu.“Yule kijana akiwa amejificha huku macho yakiwa kwenye nyumba ya mwanamke huyo, ghafla alimwona mwanaume mwingine akifika nyumbani hapo na kugonga mlango.
“Mwanamke alifungua mlango na kuondoka na mwanaume huyo. Ndipo Nyamkinda alitoka pale alipokuwa amebana na panga lake na kumvamia kisha kuanza kumcharanga hovyo mwanamke huyo na kumsababishia majeraha makubwa,” alisema shuhuda mmoja.
“Sisi tulisikia kelele kutoka nyumbani kwa Bahati, tulipofika tulimkuta anagaragara chini huku akitokwa na damu nyingi mwilini na akilia kwa uchungu.“Tulipomuuliza kulikoni alisema amecharangwa mapanga na hawara yake wa zamani baada ya kumwona akiondoka na mwanaume mwingine, hivyo tukampa msaada wa kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Butiama ambako amelazwa,” aliongeza shuhuda huyo.
Afisa mmoja wa polisi mjini Butiama ambaye ameomba jina lake lisitajwe kwa kuwa siyo msemaji, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, mtuhumiwa huyo anasakwa baada ya kutokomea kusikojulikana.
Post a Comment