Jopo la mahakimu watatu likiongozwa na Hakimu John Utamwa, Ignas Kitusi na Eva Nkya liliwaachia washitakiwa hao baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa hao.
Mbali na Maranda washitakiwa wengine walioachiwa huru ni Farijala Hussein na waliokuwa wafanyakazi wa BoT, Ester Komu, Bosco Kimera na Imani Mwakosya.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Utamwa alisema washitakiwa waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka manne kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo BoT na wiziwa Sh milioni 207.2 wako huru kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka hayo bila kuacha shaka kama inavyotakiwa kisheria.
Alisema upande wa Jamhuri umeshindwa kuithibitishia mahakama jinsi Maranda na Farijala walighushi makubaliano ya kukusanya deni kati ya Kampuni ya General Marketing ya India kwenda Kampuni ya Rashas (T) ya Tanzania.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa bila Mwakosya kuwepo mahakamani, Hakimu Utamwa alisema upande wa Jamhuri wameshindwa kumleta mpelelezi wa kesi hiyo ili aweze kuithibitishia Mahakama saini ambazo zinadaiwa kuwepo katika makubaliano hayo hivyo udhaifu huo hauwezi kuwatia washitakiwa hatiani.
Aliongeza kuwa, upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha shitaka la kughushi, kwa hiyo shitaka la kuwasilisha nyaraka za uongo litakuwa limekufa,kwa sababu wameshindwa kuonesha kweli nyaraka ni za kughushi.
Aidha alisemwa wameshindwa kuonesha ni jinsi gani fedha hizo zilihamishwa kama wanavyodai kuwa mchakato huo ulifanikiwa kwa sababu Maranda na Farijala walitumia nyaraka za kughushi.
“Hakuna shahidi aliyeweza kutoa ushahidi ukaenda sawa na hati ya mashitaka iliyofunguliwa mahakamani hapo dhidi ya washitakiwa,” alisema Hakimu Utamwa.
Nyaraka zinazodaiwa kughushiwa ni hati za makubaliano ya kuhamishiwa deni kutoka Kampuni ya General Marketing ya India kwenda Kampuni ya Rashas (T) ya nchini Tanzania, ambazo walizutumia na kuiba fedha hizo.
Baada ya Hukumu hiyo, Farijala alirudishwa rumande kwa sababu anatumikia kifungo cha miaka miwili jela alichohukumiwa katika kesi nyingine na Maranda aliachiwa lakini bado ataendelea kwenda mahakamani kwa kuwa anakabiliwa na kesi nyingine.
Ndugu na marafiki waliokuwepo katika eneo hilo la mahakama walishukuru mahakama kutoa uamuzi wa haki na kusema kweli Mungu ametenda miujiza.
chanzo; (http://www.udakuspecially.com/2015/07/hii-nayo-mpya-watuhumiwa-wa-epa.html)
Post a Comment