Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana alikana kutoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwamba mtoto, hana akili na mpuuzi.
Askofu
Gwajima alikanusha tuhuma hizo wakati akisomewa maelezo ya awali mbele
ya Hakimu Mkazi wa Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo, alidai kuwa kati ya Machi 16 na
25, mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers, vilivyopo Kawe
jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alitoa lugha ya matusi kwamba ‘mimi
Askofu Gwajima nasema askofu Pengo ni mpuuzi mmoja yule, mjinga mmoja,
amekula nini yule, sijui amekula nini yule mtoto hana akili yule’
alinukuu maneno hayo.
Alidai
kuwa Askofu Gwajima alitoa maneno hayo yakufadhaisha dhidi ya Askofu
Pengo na kwamba yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Upande
huo wa Jamhuri ulidai kuwa Machi 27, mwaka huu mshtakiwa alifikishwa
Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.
Ilidaiwa kuwa alifunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma hizo.
Hata
hivyo, Askofu Gwajima alikana mashitaka hayo lakini alikiri majina
yake, wadhifa wake, kuhojiwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, kweli kanisa lake liko Kawe na kushitakiwa mahakamani hapo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa unatarajia kuita mashahidi saba na watawasilisha vielelezo vitano.
Wakati
huo huo, mahakama hiyo imepiga kalenda kusoma maelezo ya awali ya kesi
inayomkabili askofu huyo na wenzake watatu, baada ya mshtakiwa wa nne
kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Hakimu Dyansobela Agosti 10, mwaka huu.
Mbali na Gwajima wengine ni anayedaiwa kuwa mlinzi wake George Mzava,Yekonia Bihagaze na Georgey Milulu.
Katika
kesi ya msingi, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Machi 29,
2015 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, jijini Dar es
Salaam,washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakimiliki bastola aina ya
Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa
mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.
Alidai
kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 32 (1)
na cha 34 (1)(2) na(3) cha sheria ya Silaha na Milipuko sura ya 223
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Upande
wa Jamhuri, uliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio Mzava akiwa na
wenzake hao walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola
pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun. Washtakiwa walikana
mashitaka yao kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana.
Post a Comment