Ule usemi wa kwamba milima haikutani, binadamu hukutana umejidhihirisha baada ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, kukutana uso kwa uso na aliyekuwa mchumba’ke, Penniel Mwigilwa ‘Penny’ kwenye shughuli ya 40 ya mtoto wa mwigizaji, Aunt Ezekiel hivyo kupata fursa ya kukumbushia enzi zao.
Tukio hilo lililoshuhudiwa na Ijumaa Wikienda lilijiri wikiendi iliyopita nyumbani kwa Aunt, Mwananyamala, Dar ambapo pati hiyo ilihudhuriwa na mastaa kibao.
Katika tukio hilo, Diamond ndiye aliyeanza kumuona Penny akamwita kwa lengo la kumsalimia ambapo naye alitii akionekana mwenye furaha kisha walikumbatiana huku baadhi ya waalikwa wakiwataka kukumbushia enzi za mapenzi yao.
Baada ya salamu, waliendelea kuzungumza ‘mambo yao’ huku muda wote wakicheka.
Baadaye, Penny aliwasalimia baadhi ya watu waliokuwa wamekaa na Diamond na kwenda kukaa pembeni yao huku akitazamana na Diamond kwa shauku kubwa.
Ijumaa Wikienda liliendelea kufuatilia kila jambo juu ya wawili hao ambapo muda mwingi walikuwa wakitaniana huku Romy Jones akichagiza utani huo.Hata hivyo, baadaye Romy alinyanyuka alipokuwa ameketi na kwenda kwa Penny kama mtu aliyeagizwa jambo na Diamond ambapo walizungumza kwa kirefu.
Alipoulizwa Penny kulikoni yeye na Diamond kuwa gumzo mahali hapo, alisema kuwa hana sababu ya kununa maana hakuna kibaya ambacho kipo kati yake na jamaa huyo kwani wamekuwa wakiwasiliana na kuongea vizuri ingawa kila mtu ana mambo yake.
“Hapa tumealikwa na kila mtu amekuja kivyake, sasa si rahisi ukawaona watu usiwasalimie au uchukie maana hakuna sababu ya kufanya hivyo, sina ugomvi na Diamond na sina mipaka yoyote ya kusalimiana au kuongea naye,” alisema Penny.
Kwa upande wa Diamond alisema kuwa alikuwa pale kwa ajili ya kufuturu na kumfurahia kila mtu hivyo hakuna dhambi yoyote kwake kusalimiana na Penny.
Post a Comment