USIOMBE yakukute! Beatrice Nyato au mama Prisca, mkazi wa Kurasini, Dar, anapika, anapakua na kulala nje ya nyumba yake baada ya kutupiwa vyombo nje na mtu aliyemtaja kwa jina moja la Anwar ambaye ni mkurugenzi wa kampuni moja ya usafirishaji ya jijini Dar.
Beatrice Nyato au mama Prisca, mkazi wa Kurasini, Dar, anayepika, anapakua na kulala nje ya nyumba yake.
Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita, mama Prisca alisema kasheshe hiyo ilimkumba yeye na wapangaji wake.Alisema awali alikwenda katika ofisi za mkurugenzi huyo kwa lengo la kuuza nyumba yake ili amlipie mume wa binti yake deni la benki ambapo yeye ndiye alimdhamini kupitia nyumba hiyo.
Vitu vya familia hiyo vikiwa nje ya nyumba.
“Nilisikia ile kampuni huwa inanunua nyumba. Nilipofika, tukaongea na
mkurugenzi, akanipa mtu nije naye ili aione. Nyumba yangu ni kubwa, ina
vyumba kumi na sehemu ambayo unaweza kupaki magari madogo hata kumi.“Yule mtu alipoiona akaenda kumwambia bosi wake, kesho yake naye akaja kuiona. Kuhusu bei, nilimwambia Sh. milioni 600, yeye akasema parefu. Nikashuka hadi Sh. milioni 500, akasema atanipa Sh. milioni 400 lakini baadaye akasema atanipa milioni 320 ili milioni 80 iwe kwa ajili ya kuhamisha wapangaji, bili ya maji na umeme. Nikakubali,” alisema mwanamke huyo.
Mama Prisca alisema, waliandikishiana kwenye karatasi kwa makubaliano ya kuanza kulipa pesa anazodaiwa benki, zinazobaki kumlipa kupitia cheki.
Bosi huyo, kwa mujibu wa mama Prisca, aliahidi kuanza kulipa shilingi milioni 150 kwa ajili ya benki (jina lipo) na nyingine angemalizia baadaye.
Prisca, mkazi wa Kurasini, Dar, akipika nje ya nyumba yake.
“Siku kadhaa mbele alinipigia simu akasema atanipa afisa niende naye
benki kwa ajili ya kufuatilia hati kwa kuwa yeye atakuwa safirini.
Nikaambiwa mimi na mkwe wangu tuandike barua iende benki. “Baada ya wiki mbili nikapigiwa simu na benki kuwa deni la Sh. milioni 50 limeshalipwa.
“Kulikuwa na deni la pili, benki nyingine, mkurugenzi akasema hawezi kulipa bila mimi kutoa hati ya nyumba, nikampa, akalipa benki Sh. milioni 70,” alisema mama huyo.
Mama Prisca alikuwa akiendelea kudai Sh. milioni 80 ambayo walikubaliana ilipwe kupitia cheki lakini alipokwenda kwa ajili ya kujaza fomu ili aingiziwe fedha yake hiyo alishangaa kuambiwa malipo yameishia pale na hakuna zaidi ikiwa na maana kwamba, nyumba ilinunuliwa kwa Sh. milioni 270 tu!
“Nilimfuata tena, akaja juu, akasema nataka nini tena? Huku akinitolea maneno makali kuwa yeye ni mgonjwa nampigia kelele, akasema niondoke asije akaniitia polisi.
“Hivi karibuni, sijui siku gani ile! Saa 5:00 asubuhi, walikuja watu waliojitambulisha kuwa wanatoka kampuni ya udalali wakiwa wameongozana na mabaunsa kama 10 na askari 15, wakadai wametumwa na aliyenunua nyumba kuibomoa.
“Mimi sikuwepo, hata wapangaji walikuwa kwenye shughuli zao, lakini kaka yangu alikuwepo. Aliwazuia kwa kuwataka waende kwanza serikali za mtaa lakini wakagoma.
“Kaka alinipigia simu na kunipa taarifa, nikachanganyikiwa, nikakumbuka nina fedha ndani, nikamwambia atoe mfuko wenye fedha, akasema haupo ila mimi nifanye ninavyoweza niwahi.
“Nilipofika, niliwakuta mabaunsa na polisi wenye silaha wameizingira nyumba. Nikazuiliwa kuingia kwa kuambiwa kuna kazi inaendelea.
“Majirani zangu wakaja kunivuta pembeni na kuniambia mama Prisca utazimia utupe kazi ya kukupepea au utakufa kwa presha. Nikakaa pembeni wakinipepea, baadaye wakaniondoa kabisa eneo lile.
“Wakati naondoka, nikampigia simu wakili wangu, akaniambia suala langu linatakiwa lifikishwe mahakamani. Mpaka leo ni siku ya 10, tunalala hapa nje, ndani kuna walinzi wenye silaha, wanaingia kwa shifti. Geti limefungwa na mnyororo.
“Wapangaji nao baada ya kukuta vyombo vyao vipo nje wakapaniki, wakasema watanipiga vinginevyo niwape fedha ya kulala gesti na fedha ya chakula. Jumanne iliyopita wakanipeleka Kituo cha Polisi Chang’ombe, nikalala siku moja, siku ya pili nikapelekwa Kituo cha Polisi Kilwa Road nikalala, kesho yake nikatolewa kwa dhamana.
Baada ya kutoka kwa mama Prisca, waandishi wetu walikwenda kwenye ofisi za mkurugenzi huyo zilizopo Kurasini ambapo walinzi waliwazuia kuingia ndani wakidai hairuhusiwi.
Jumamosi iliyopita, waandishi wetu walikwenda tena lakini mtu mmoja aliyekataa kujitambulisba alisema ishu ya mwanamke huyo ipo polisi (bila kutaja kituo) hivyo mkurugenzi huyo hawezi kusema lolote na hakukuwa na kiongozi yeyote ofisini hapo.
Post a Comment