INASIKITISHA! Mmiliki wa Shule ya Msingi na Awali (International) ya Mount Zion iliyopo Bahari Beach, Dar, Annah Mizighi Mwambili, 47, (pichani) ameuawa na mwili wake kutupwa ndani ya shule yake baada ya kupotea kwa zaidi ya miezi sita huku mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Tatu Ntimizi, Said Ntimizi akidaiwa kuwa mmoja kati ya watuhumiwa wa mauaji hayo.
Duru za awali za upelelezi wa polisi, zinamtaja Said kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na marehemu bila kufafanua alihusikaje na mauaji hayo ya kinyama yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana, siku na tarehe isiyojulikana na mwili wake kutupwa kwenye shimo la maji taka ndani ya eneo la shule aliyokuwa akiimiliki.
Aidha, nyuma ya taarifa hiyo ya mauaji, deni la shilingi milioni mia tisa (900,000,000) ambalo mwanamke huyo alikuwa akimdai mmoja kati ya watuhumiwa hao ambao majina yao yote bado hayajafahamika likitajwa kuwa ndiyo chanzo cha Annah kutolewa uhai.
ALIANZA KWA KUTOWEKA
Wakisimulia kwa uchungu namna Annah alivyotoweka nyumbani kwake, ndugu wa marehemu walisema, awali Desemba 26, mwaka jana kwenye Sikukuu ya Boxing Day, kuna wageni walifika nyumbani kwake, Boko, Dar, wakazungumza na baadaye wakaondoka naye na hakurudi tena.
NDUGU WAPATA WASIWASI, WATOA TAARIFA POLISI
Ndugu hao walisema kuwa siku za kwanza hawakupata wasiwasi kwa vile ilikuwa kawaida ya marehemu kuwa mtu wa safari kutokana na biashara zake na kuongeza kuwa walianza kupata wasiwasi baada ya siku nne kupita huku kukiwa hakuna mawasiliano kati yao na marehemu, jambo lililowalazimu kuripoti Kituo cha Polisi cha Wazo Hill ambao walianza uchunguzi.
WAUMINI WAFUNGA NA KUSALI
Wakati wote huo, waumini wa kanisa alilokuwa akisali marehemu Annah la Winners Chapel lililopo Ukonga jijini Dar waliamua kufanya maombi ya kusali na kufunga kwa ajili ya kumuomba Mungu awaoneshe mpendwa wao alipo.
MAITI YAPATIKANA SHULENI KWAKE MIEZI 6 BAADAYE
Kwa masikitiko makubwa, ndugu hao walisema, Juni 22, mwaka huu, ikiwa ni miezi sita na siku na chache tangu kupotea kwa ndugu yao, walipata taarifa iliyowashtua na kuwaumiza, kwamba mwili wa mpendwa wao umepatikana ukiwa umeharibika vibaya ndani ya shimo la maji machafu katika shule yake.
HABARI ZA CHINICHINI
Habari za chinichini ambazo si rasmi zilizonyakwa na Gazeti la Uwazi, zinaeleza kuwa baada ya marehemu huyo kuchukuliwa nyumbani kwake, inadaiwa watuhumiwa walikwenda naye mpaka kwenye nyumba ya mganga mmoja maarufu wa kienyeji (jina kapuni) ambako walimuua kisha kuuchukua mwili wake na kuutupa shimoni.
POLISI WANASA TUKIO
Kama Waswahili wasemavyo, damu nzito kuliko maji ndivyo ilivyokuwa kwa Annah ambaye damu yake iliendelea kuwasumbua wahusika kiasi cha unyama wao kuwafikia polisi kupitia njia za kijasusi na hivyo kufanikiwa kumnasa mmoja wa watuhumiwa.
“Polisi walipopata taarifa za mauaji hayo, waliamua kufuatilia, wakabaini mmoja kati ya watuhumiwa hao yuko Arusha. Wakamuwekea mtego na kufanikiwa kumnasa, wakamleta jijini Dar ambapo aliwataja aliodai kushirikiana nao,” chanzo kutoka vyombo vya usalama kililiambia Uwazi.
MWALIMU MKUU AZUNGUMZA
Akizungumza na Uwazi, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Dony Maige alisema shule yake ilikuwa imefungwa wakati marehemu ambaye ni mmiliki na mkurugenzi akiwa hajulikani alipo.
“Januari mwaka huu, tarehe za mwanzoni tulifungua shule kama kawaida baada ya likizo ya Desemba ambapo wanafunzi waliendelea na masomo. Lakini bajeti ilikuwa ngumu kutokana na mkurugenzi ambaye ndiye mtoaji wa fedha za matumizi ya shule na malipo ya wafanyakazi, kutoonekana.
“Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wazazi kulazimika kuchangia huduma nyingine muhimu japokuwa walikuwa wamemaliza ada za watoto wao.
MWALIMU AWATOA MACHOZI WAOMBOLEZAJI
“Juni 21, mwaka huu tukiwa tumefunga shule na kutarajia kufungua tena kwa ajili ya muhula mpya wa masomo, ndipo nilipopokea simu kutoka vyombo vya usalama na kunitaka kusitisha zoezi la kufungua shule kwa kuwa kutakuwa na oparesheni maalumu katika eneo la shule. Nikaambiwa niwaondoe wafanyakazi wote isipokuwa mimi peke yangu.
“Nilishangaa, baada ya kufika shuleni na kuwaona polisi wakiwa eneo la tukio. Nilishtuka kutokana na maswali waliyokuwa wakiniuliza. Lakini jambo lililonishtua zaidi ni kuuona mwili wa marehemu Annah ukitolewa ndani ya shimo la maji machafu lililopo ndani ya shule ambayo kwa miezi yote sita wanafunzi na hata sisi walimu tulikuwa tukipita bila kujua.
“Kwa kweli sijawahi kukutana na kipindi kigumu kama hiki katika maisha yangu. Ni jambo la ajabu sana. Nimejiuliza maswali mengi na kukosa majibu,” alisema mwalimu huyo huku waombolezaji wakishindwa kuzuia machozi yaliyokuwa yakiwatiririka.
MWILI WAAGWA BILA KUFUNULIWA
Wakati wa kuuaga mwili huo, Jumamosi iliyopita nyumbani kwa marehemu, waombolezaji walitoa heshima zao za mwisho kwa masikitiko mbele ya jeneza la marehemu bila kufunuliwa kutokana na mabaki ya mwili huo kuharibika vibaya.
Mwili wa marehemu Annah ulipumzishwa katika Makaburi ya Kwakondo, Ununio jijini Dar. Hakika bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake libarikiwe. Amina. Marehemu ameacha watoto watatu, Steven, Irene na Emerly Mwambili.
POLISI KINONDONI WALIVYOSEMA
Uwazi lilimpigia simu Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Emanuel Mlei na kumuuliza yafuatayo.
Uwazi: “Kuna madai kwamba, mtoto wa aliyewahi kuwa waziri kwenye serikali ya awamu ya tatu, Tatu Ntimizi, Said Ntimizi mnamshikilia kwa mauaji ya mwanamke aliyekuwa mmiliki wa shule, Annah Mwambili, ni kweli?”
Kamanda: “Kuhusu hilo siwezi kulisema kwa sasa. Ila kesho (jana) nenda pale kwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova ataliongelea yeye.”
Uwazi bado liko kazini kuchimba tukio hili la kinyama na kwamba litaendelea kuwaletea mapya kadiri yanavyopatikana.
Chanzo; (http://www.globalpublishers.info/profiles/blogs/huyu-ndiye-anayedaiwa-kuuawa-ma-mtoto-wa-waziri)
Post a Comment