WAKATI wafuasi
wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi ( Ukawa)
wakiwa na shangwe kutokana na kumpata Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kama mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, ugumu
wa kiongozi huyo kuingia ikulu umebainishwa, Uwazi lina habari kamili.
Ingawa aliripotiwa kuwa na wafuasi wengi
akiwa CCM, ushahidi unaonesha kuwa siyo mashabiki wake wote
wamefurahishwa na hatua yake ya kuhamia upinzani, hivyo idadi kubwa ya
wapiga kura aliokuwa akiwategemea, wameamua kuachana naye na wao
kuendelea kubakia chama tawala.
Ugumu mwingine, unatokana na ukweli kuwa
licha ya Chadema kujizatiti hadi vijijini, lakini haina mtandao mpana
kama ilivyo kwa CCM, hivyo hata ile ‘amsha amsha’ inayoonekana mijini
hivi sasa, haiko vijijini, ambako chama tawala bado kina mizizi na kina
wapiga kura wengi maeneo hayo.
Jambo lingine linalotajwa kuwa ni gumu
kwa Lowassa kuingia ikulu, ni ukweli kuwa kujiweka kando kwa viongozi
wawili waliokuwa na mashabiki wengi, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.
Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wa Cuf, Profesa Ibrahim Lipumba
kumewachanganya mno wafuasi wao na hivyo kuwa njia panda.
Ukimya wa Dk. Slaa, anayeaminika kufanya
kazi kubwa ya kuwashawishi watu kuipenda Chadema, umewafanya baadhi ya
wafuasi wake kutokuwa na mwelekeo, hivyo kuweka uwezekano mkubwa wa watu
hao ama kupiga kura kwa wagombea wa vyama vingine au wasipige kabisa,
kitu kitakachopunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya kura za Lowassa
kuelekea ikulu.
Post a Comment