Mgombea ubunge jimbo la Shinyanga mjini Patrobas Katambi aliyechaniwa fomu zake leo asubuhi mjini Shinyanga
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo ofisini kwake
Ikiwa leo ni siku ya kurudisha fomu za kugombea ubunge na udiwani, mgombea ubunge jimbo la Shinyanga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi Ukawa Patrobas Katambi ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema taifa amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuvamiwa na kundi la watu saba kisha kuchaniwa fomu zake za ubunge. Tukio hilo la aina yake limetokea saa 2 na dakika 45 asubuhi katika eneo la Ibinzamata mjini Shinyanga katika barabara ya Shinyanga kuelekea Tinde.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha amesema tukio hilo limetokea wakati mgombea huyo akiwa amepanda kwenye gari lililokuwa linaendeshwa na Albert Katambi lenye namba za usajili T.781 AKT Toyota Rav 4 kugongwa na gari aina ya Noah nyeusi kisha kuvamiwa na kundi la watu saba.
"Mgombea huyo na dereva wake walikuwa wanaelekea kituo kikubwa cha mabasi mjini Shinyanga,ghafla gari lao likagongwa kwa nyuma na gari aina ya Noah nyeusi ambayo haikufahamika namba zake mara moja,watu hao walishuka kwenye Noah hiyo kisha kulizunguka gari hilo na kuchukua fomu za mgombea zilizokuwa sehemu ya mbele ya kioo cha gari (Dashboard) na kuzichana chana",amesema Kamanda Kamugisha.
Amesema pamoja na kuchana fomu hizo watu hao pia walichukua shilingi 2.5 milioni mali ya Patrobas Katambi alizokuwa ameziweka kwenye droo ya gari na kutokomea nazo kusikojulikana na kwamba mgombea aliwatambua watu hao kwa sura.
Amesema jeshi la polisi linafanya uchunguzi wa tukio hilo la kuharibu mali za mgombea huyo wa ubunge ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watuhumiwa.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Shinyanga Mjini Titus Jilungu amesema fomu zilizoharibiwa ni nakala za fomu za mgombea(photocopy) na siyo nakala halisi huku akiwataka wafuasi wa chama hicho kutokata tamaa na kuendelea kumlinda mgombea huyo kwani lulu kubwa kwa mkoa wa Shinyanga.
Jilungu amesema wanachokifanya hivi ni kukamilisha zoezi la kurudisha fomu za mgombea huyo na mambo yanaendelea vizuri.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Taarifa zaidi tutawaletea hivi punde.......Endelea kutembelea Malunde1 blog,Fahari ya Shinyanga kwa tunafuatilia zaidi juu ya tukio hilo.
Post a Comment