Mganga anayedaiwa kufumaniwa na mke wa mtu.Na Victor Bariety, Geita
MWANAUME mmoja mkazi wa mtaa wa Mkoani kata mpya ya Bombambili wilayani Geita, mkoani Geita ambaye ni mganga wa kutibu mifupa ya binadamu iliyovunjika, amenusurika kifo baada ya kufumaniwa akidaiwa kufanya mapenzi na mke wa mtu.
Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Masatu Mafulu (40) alikutwa akifanya mapenzi na mwanamke aliyetajwa kwa jina la Pendo Simon (36), ambaye ni mke wa Thomas Samweli Mapunda (46) wote wakazi wa mtaa huo wa Mkoani.
Tukio hilo lililovuta umati mkubwa wa watu, lilitokea Julai 26, mwaka huu majira ya 8:36 mchana kwenye nyumba ya wageni ijulikanayo kwa jina la Masunga iliyopo Mtaa wa Kisesa kata ya Kalangalala jirani na Kanisa Kuu la Roman Catholic (RC).
Mapunda ambaye ni mume wa mwanamke aliyefumaniwa, akizungumza mbele ya viongozi wa polisi jamii Mtaa wa Kisesa alidai kuwa, mwanamke huyo wamezaa naye watoto wanne na ameishi naye kwa zaidi ya mika 16.
Aliongeza kuwa, siku ya tukio alipata taarifa za mkewe kuingizwa kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni kutoka kwa watu wake wa karibu na kuchukua jukumu la kutaarifu polisi jamii na baadaye waliongozana naye hadi eneo la tukio hilo.
“Tulipofika hawa polisi jamii waligonga kwenye chumba tulichoelekezwa wamo na kweli sikuamini baada ya kukuta ni mke wangu, roho iliniuma sana hata wananchi wa eneo hilo walichukizwa na kitendo hicho wakataka kumshambulia lakini tuliwazuia maana sheria zipo,’’ alisema Mapunda kwa masikitiko.Alisema, polisi jamii waliwakamata mwanaume huyo na mkewe hadi zilipo ofisi zao na baadaye waliwataarifu polisi waliofika eneo hilo na kuwachukua ili wasishambuliwe na watu ambao walikwishajikusanya eneo hilo wakimtaka mgoni huyo ili wamchome moto.
Hata hivyo, baada ya kufikishwa polisi mtuhumiwa huyo alimzunguka na kumfungulia kesi ya kujeruhi ili kutaka kumdhoofisha asifuatilie kesi ya ugoni.
“Nipo polisi eti jamaa amenifungulia kesi ya kumjeruhi wakati siku ya tukio sisi ndiyo tuliokuwa tunazuia watu wasimpige, anataka kunidhoofisha wakati tayari amenivunjia ndoa yangu maana mke wangu nilikuwa nampenda na tayari nimekwishazaa naye watoto wanne,’’ alisema.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kalangalala, Hamad Hussein alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa, baada ya kuonekana kuna hatari ya kutokea uvunjifu wa amani kwenye ofisi hizo za polisi jamii, aliagiza waitwe polisi ambao waliwachukuwa watuhumiwa hadi kituoni.
Post a Comment