Kwa ufupi
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa miongoni mwa
mambo yanayoleta hofu na kusababisha presha kuongezeka kila kukicha ni
woga wa kufanya makosa katika uteuzi wa ndani, hali inayoweza
kukigharimu chama hapo baadaye hasa kutokana na kuongezeka nguvu ya
upinzani.
Dodoma/Z’bar. Wakati vikao vya
juu vya CCM vya kuchuja wagombea urais vikianza leo, hofu na wasiwasi
umezidi kutanda miongoni mwa wagombea, viongozi na wanachama wa chama
hicho kuhusu namna ya kuikabili minyukano baina ya wagombea hao na
kibarua cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa miongoni
mwa mambo yanayoleta hofu na kusababisha presha kuongezeka kila kukicha
ni woga wa kufanya makosa katika uteuzi wa ndani, hali inayoweza
kukigharimu chama hapo baadaye hasa kutokana na kuongezeka nguvu ya
upinzani.
Kutokana na hali hiyo kumekuwa na shinikizo kutoka
katika makundi mbalimbali chama hicho kuwa makini kumteua mgombea
anayekubalika, msafi na mwenye kuchagulika ambaye atatoa ushindani kwa
wagombea wa upinzani, hasa Ukawa.
Vilevile, kumekuwapo na wasiwasi wa baadhi ya
wagombea kutishia kukihama chama hicho endapo majina yao yatakatwa,
jambo ambalo pia linakiweka njia panda.
Nape: Hakuna shinikizo
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye amejibu hoja hizo akisema chama hicho hakitafanya uamuzi kwa
kushinikizwa na watu, bali kitafuata taratibu na kanuni.
“Tunazo taratibu, tunazo kanuni zetu. Nataka
kuamini kuwa kila mtu aliyegombea anajua kuna kushinda na kuna kushindwa
na kuna kuteuliwa na kutokuteuliwa,” alisema jana alipozungumza na
waandishi wa habari.
Alisema hataki kuamini kuwa kuna mgombea kati ya 38 walioomba nafasi hiyo ambaye anaamini anaingia kushinda tu.
“Usipokuwa wewe anakuwa mwingine... Asiyekubali
kushindwa basi atakuwa si mshindani. Usisahau hizo ni presha za wapambe
hazitupi tabu. Tunachojua walioshindwa watapeana mkono na aliyeshinda na
chama kitabaki kuwa kimoja,” alisema Nape.
Alisema wananchi waamini chama kitatenda haki, taratibu zitafuatwa na kuwapa mgombea bora.
“Haya ni maneno ya presha za barabarani
ninachoamini mwisho wa siku hakuna fujo, hakuna vurugu, vyombo
vimejipanga vizuri hakuna vurugu na wapambe kusindikizana ni jambo la
kawaida,” alisema na kuongeza kuwa anafahamu kuwa wapo watakaohuzunika
kutokana na majina ya watu wao kukatwa lakini hakuna jinsi kwa sababu
kanuni za CCM zinasema Kamati Kuu (CC) itapendekeza majina matano kwa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Pia kanuni hizo zinasema NEC itapendekeza majina matatu kwa mkutano mkuu ambao utachagua mmoja.
Post a Comment