Katika
siku ya jana kulikuwe na minong’ono ya hapa na pale iliyokuwa imeenea
katika korido za Makao Makuu ya CCM na viunga vya mji wa Dodoma, ikidai
kuwa jina la mwanasiasa huyo halitakuwemo katika orodha ya majina ya
tano bora itakayopelekwa ndani ya NEC kutoka Kamati Kuu.
Minong’ono
hiyo ya kuwepo uwezekano wa jina la Lowassa kutotoka Kamati Kuu,
iliongeza hofu zaidi miongoni mwa wapambe wa mwanasiasa huyo, baada ya
mwanasiasa mkongwe nchini anayejulikana wazi kuwa katika kambi ya
mgombea huyo, Kingunge Ngombale-Mwiru kutinga katika Ofisi za Makao
Makuu ya chama hicho mchana wa kati ya saa 8:00 na saa 9:00.
Baada ya kushuka kwenye gari lake na kuelekea moja kwa moja katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Kingunge alisikika akisema “Nina miadi ya kuonana na Katibu Mkuu saa 8.30 mchana huu, ameniita.”
Mwanasiasa
huyo ilimchukua takriban saa nzima akiwa katika ofisi ya Kinana.
Alipotoka tu nje, kada mwingine wa CCM, Hamis Mgeja, ambaye ni
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Shinyanga aliingia katika ofisi ya
Kinana akidaiwa kuitwa pia.
Mgeja,
kama ilivyo kwa Kingunge, ni miongoni mwa makada wa CCM ambao wamekuwa
wakijipambanua wazi wazi kuwa katika kambi ya Lowassa kiasi cha makada
hao kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mgombea huyo wa kutafuta
wadhamini 450 katika mikoa 15 ya Tanzania, kati ya hiyo mitatu ikiwa ni
ya Zanzibar.
Haikuweza
kufahamika kwa undani ni kwanini makada hao wa CCM waliitwa na Kinana
ofisini kwake, lakini baadhi ya wadadisi wa mambo walielezea tukio hilo
kama sehemu ya juhudi za kambi hiyo ya Lowassa kuokoa jahazi la mgombea
wao huyo jina lake kuondolewa mapema na Kamati Kuu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ratiba ya awali ya mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, vikao hivyo muhimu katika mchakato huo vilitarajiwa kufanyika juzi na jana, lakini vikao vyote viwili hivyo havikuweza kufanyika kama vilivyopangwa, huku kukiwa hakuna taarifa yoyote rasmi kwanini havikufanyika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ratiba ya awali ya mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, vikao hivyo muhimu katika mchakato huo vilitarajiwa kufanyika juzi na jana, lakini vikao vyote viwili hivyo havikuweza kufanyika kama vilivyopangwa, huku kukiwa hakuna taarifa yoyote rasmi kwanini havikufanyika.
Kwa
kawaida kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ambacho huongozwa na
Rais Kikwete mwenyewe akisaidiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahiman
Kinana, ndicho kinachotoa dira ya mwelekeo kwa wajumbe wa Kamati Kuu,
kikao ambacho kina mamlaka ya kuteua majina matano kutoka miongoni mwa
wote waliojitokeza kuomba nafasi hiyo.
Kikao
hicho cha Kamati ya Usalama na Maadili ndicho kinachopokea majina ya
wote waliojitokeza kuomba nafasi hiyo, kabla ya kujadili mienendo ya
kimaisha ya kila mmoja wa wagombea, hasa katika suala zima la kimaadili
na uzingatiaji wa miiko na viapo vya utii kwa chama hicho.
Baada
ya Kamati hiyo kukamilisha kazi hiyo, majina yote ya walioomba uteuzi
huo huwasilishwa ndani ya kikao cha Kamati Kuu, kila jina likiwa
limetendewa haki kwa kubeba maelezo ya sifa za miendendo hiyo ya
kiamaadili na uzingatiaji huo wa miiko na viapo vya utii kwa Chama,
kabla ya kikao hicho kuteua majina matano yanayopelekwa kwenye kikao cha
Halmashauri Kuu (NEC) kwa hatua zaidi.
Kutofanyika
kwa vikao hivyo muhimu katika mchakato huo wa uteuzi ndani ya CCM hadi
jana kama ilivyokuwa imepangwa awali, kwa kiasi fulani kumeongeza hofu
na kukoroga vichwa vya baadhi ya wapambe wa wagombea wa urais kutokana
na kutofahamu sababu na malengo ya kuahirishwa huko kwa vikao hivyo.
Hadi
jana jioni ya Julai 9, 2015, vikao hivyo muhimu viwili vinavyoongozwa
na Rais Kikwete mwenyewe, havikuwa vimefanyika kutokana na kile
kilichoelezwa na watu wa karibu na kiongozi huyo mkuu wa nchi na chama
chake hicho kwamba ni kukabiliwa na majukumu mengine mazito ya kitaifa.
Kwa
siku ya jana Alhamisi pekee, Rais Kikwete alikuwa na jukumu la kuzindua
ukumbi wa kisasa wa Mkutano Mkuu wa CCM uliojengwa kwa gharama za chama
hicho katika eneo lililopo karibu na majengo ya Ofisi za Hazina Ndogo
mjini Dodoma, hafla iliyofanyika kuanzia asubuhi hadi mchana kabla ya
alasiri kiongozi huyo kwenda kulihutubia Bunge na kufunga shughuli za
Bunge la Bajeti.
Katika
korido na viunga vya Ofisi za Makao Makuu ya CCM pamoja na maeneo ya
Dodoma Hotel na NAM Hotel ambako wengi wa wapambe hao wa Lowassa
wamechukua vyumba kwa ajili ya malazi, wengi wao walikuwa wakionyesha
nyuso za huzuni, huku wakionekana kuchanganyikiwa bila kufahamu ni nini
hasa kilichokuwa kikiendelea ndani ya chama hicho.
Post a Comment