Wema Sepetu |
Inasikitisha! Mrembo Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ amejikuta akiangua kilio baada ya kupewa maneno ya kejeli na aliyekuwa mpenzi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kufuatia kupigwa chini kwenye kura za kuwania Ubunge wa Viti Maalum mkoani Singida kupitia Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
wemasepetuMrembo kunako Bongo movie aliyekuwa akiwania ubunge wa viti maalum Ikungi Singida, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo makini kililiambia Ijumaa Wikienda kwamba, Julai 24, mwaka huu Wema alijikuta akiangua kilio cha aina yake kufuatia maneno ya kumshambulia kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo Diamond muda mfupi baada ya kuangushwa katika kinyang’anyiro hicho cha ubunge kilichofanyika katika Wilaya ya Ikugi, Singida.
Kiliendelea kunyetisha kwa sauti ya upole kwamba, miongoni mwa vitu vilivyosababisha Wema kudondosha chozi ni pamoja na maneno ya Diamond aliyoandika muda mfupi tu katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram huku akijua wazi kwamba mwanadada huyo alishapoteza fedha nyingi ili apate nafasi ya kuingia mjengoni, Dodoma.
“Ujue watu wengi hawakujua kilichomuuma zaidi Wema ila mimi kaniambia kwamba, kilichomuuma si kukosa nafasi hiyo ila ni maneno ya Diamond aliyoandika kwenye ukurasa wake wa Instagram maana yamemchoma na hakutarajia kama ‘ex’ wake huyo angefikia hatua ya kuonesha chuki zake wazi kiasi hicho.
“Wema alikuwa na matumaini makubwa ya kuibuka mshindi kwenye mchakato huo kutokana na kujulikana kwake na namna wajumbe walivyokuwa wanampa matumaini ila hali imekuwa ndivyo sivyo.
“Baada ya matokeo, sisi tulimuona akiwa kawaida tu lakini baadaye alibadilika na kuwa mnyonge hali iliyonifanya nimuulize kisa cha kuwa vile ndipo akaniambia maneno ya kwenye mitandao yanamchoma.
KUMBE ALITUMIA FEDHA NYINGI
“Unajua amekuwa wa mwisho kwa kupata kura 90 hivyo ni wazi kuwa hana chake tena katika kuwania nafasi hiyo na alitumia fedha nyingi kwenye kuomba kura kwa wanachama (haikufafanuliwa kivipi kwa madai kwamba alitoa hongo), hawezi tena kuingia mjengoni kwani nafasi tatu zimechukuliwa na wenzake hao, hivyo anachotakiwa kuanzia sasa ni kujipanga ili kama itawezekana baada ya miaka mitano ijayo agombee tena,” kilisema chanzo hicho.
WEMA ANASEMAJE?
Ijumaa Wikienda, kama kawaida yake, baada ya kupata ‘unyunyuzi’ huo lilimtafuta Wema ili aweze kuanika hisia zake baada ya matumaini yake kuishia njiani ambapo alisema kwamba anaamini kila jambo limepangwa na Mungu hivyo haikuwa bahati yake zaidi ataendelea kujipanga kwa kipindi kingine.
“Namuachia Mungu maana kila jambo hupangwa na yeye, hakuna mtu anayeshindana akashindwa halafu awe ‘happy’ tu, nimeumia isipokuwa Mungu ndiye jibu la kila kitu,” alisema Wema na kuongeza:
“Nilipoamua kugombea nilijua kuna kupata na kukosa. Awamu hii nimekosa lakini dunia inazunguka.
“Nawashukuru wote walionipinga kwa sababu waliniongezea ujasiri.”
Kwa upande wa Meneja wa Wema, Martin Kadinda aliweka ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter: “Haikuwa vile tulivyotarajia….hongera Aysharose Mattembe.”
Maneno ambayo aliyaposti Diamond yaliyomchoma Wema hadi kufikia hatua ya kumwaga chozi yalisomeka: “Sitaacha kuwashukuru Wanasinginda kwa mapenzi yenu ya dhati mliyonioneshea, Moshi tukutane Kili Home.”
Wema alikuwa ni miongoni mwa wagombea wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), katika Wilaya ya Ikungi, Singida ambapo mchakato wa kura za maoni ulifanyika Julai 24, ambapo aliambulia kura 90 akishika nafasi ya nne huku mtu wa kwanza Aysharose Mattembe alikipata kura 311, nafasi ya pili ikichukuliwa na Martha Mlata aliyezoa kura 235 na ya tatu akichukua Diana Chilolo kwa kura 182.
SABABU ZA KUSHINDWA
Wikiendi iliyopita mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa ni ishu ya Wema kukosa ubunge ambapo miongoni mwa sababu hizo ni skendo mfululizo na picha zisizokuwa na maadili zilizojaa mitandaoni na kwamba CCM kwa sasa ipo kwenye mkakati mkali wa kusimamia maadili ya chama.
Post a Comment