POLISI na askari wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Fujo (FFU) wamelazimika
kutumia mabomu ya machozi kutawanya wanafunzi wa Chuo cha Kimataifa cha
Kampala (KIU) baada ya wanafunzi wa Fani ya Afya kugoma kuondoka chuoni
hapo wakifanya mkusanyiko kulalamikia kuwa fani wanayosoma
haijasajiliwa.
Askari hao walifika na kuwatawanya wanafunzi kwa mabomu ya machozi na
maji ya kuwasha jambo lililosababisha vurugu na kupelekea baadhi ya
wanafunzi kuumia pamoja na baadhi ya wananchi waliokuwa maeneo ya jirani
na chuo.
Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi
ambao waliogopa kutajwa majina yao kwa hofu ya kufukuzwa chuo walidai
kusikitishwa na uongozi wa chuo hicho kwa kufanyiwa vurugu wakati
wanachodai ni haki yao.
“Tunaiomba Serikali isimamie jambo hili kwa kweli tunanyanyasika sana
wakati tumelipa ada kubwa na bado fani tunayosoma haijasajiliwa hii si
haki kabisa na inatia uchungu,” alisema mmoja wa wanafunzi.
Alisema wanafunzi wanalalamikia usajili wa Fani ya Afya kwa upande wa
Maabara na Famasi, kuwe na mtaala unaotambuliwa na TCU, kiwango cha ada
wanayolipa ni kubwa na pia malipo ya mitihani inayotakiwa kurudiwa na
pia waalimu wengi si Watanzania bali Waganda.
Akielezea tukio la jana alisema wanafunzi wa fani hiyo walifika hapo
kwa ajili ya kufanya mitihani yao ambayo ilikuwa ianze jana hata hivyo
kuna wenzao ambao waliwapa taarifa kuwa kuna Kamati ya Bunge ambayo
itawatembelea kujua matatizo yao hivyo wakaamua kukaa wakiimba
wakisubiri kuonana na wabunge.
“Tukiwa tumekaa tunaendelea kuimba alikuja kijana mmoja ambaye ni wa
hapo chuoni lakini si mwanafunzi alituambia tuondoke akaanza kutupiga
mawe, wanafunzi walikasirika sana lakini baada ya muda walikuja askari
na kutuambia tuondoke chuo kimefungwa,” alisema mwanafunzi huyo.
Mwanafunzi mwingine alisema kuwa baadaye waliitwa FFU na kuleta gari
la maji na kuanza kuwasambaza wanafunzi ambao walikuwa wamekusanyika
kitendo kilichowafanya wasambae na kukimbizana huku na huko huku wengine
wakiumia.
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Chuo cha KIU, Keneth Liki
alikiri kutokea kwa vurugu hizo ambapo alisema uongozi wa chuo haupendi
kuona hali hiyo ikitokea na kwamba mara kadhaa wamewaelewesha wanafunzi
kuwa taratibu zinaendelea za kusajili fani hiyo ya afya zinazolalamikiwa
lakini wanafunzi hawataki kuelewa wanaendeleza migogoro.
Post a Comment