CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa kitashinda Uchaguzi Mkuu mwaka
huu kwa sababu kina mtandao mkubwa wa wanachama kuanzia ngazi ya chini
na kwamba kufurika kwa wananchi katika mikutano ya Mgombea Urais wa
Chadema, Edward Lowassa sio ushindi, kikisema kura ni mahesabu.
Aidha,
kimesema kuwa mgombea huyo wa Chadema na umoja wa vyama vinne vya
upinzani (Ukawa), amedanganywa na wapambe wake kuihama CCM na kumkejeli
ikisema gari la wagonjwa linapaswa kuwekwa nyumbani kwake siku ya
uchaguzi kwani CCM itapata ushindi wa uhakika asubuhi.
Akitoa
taarifa kuhusu kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana katika Ofisi
Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisisitiza kuwa ushindi wa chama hicho
tawala na kikongwe hauna shaka kutokana na mtandao wake kuanzia ngazi ya
chini.
Akijibu swali kuhusu kufurika kwa wananchi katika mikutano ya mgombea huyo wa Chadema, Nape alisema:
“Kwa
walioanza siasa jana ndio watashituka. Mwaka 2010 Slaa (Dk Willibrod)
katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni Mbeya alipata watu wengi kuliko
wale aliopata Edward. Lakini kura alizopata Mbeya utashangaa.
“Kupata
watu wengi mkutanoni hakutushangazi kwani kura ni mahesabu, hawa
(Chadema na mgombea wao) wanatoka pointi moja kwenda nyingine. CCM ina
mtandao, ukiondoka mjumbe wa nyumba kumi anapitia watu wake anasafisha
nyayo zenu,” alisema kiongozi huyo.
Nape
aliongeza kuwa wapinzani wote wametoka ndani ya CCM kuanzia kwa
Augustino Mrema mwaka 1995 na hadi katika chaguzi nyingine zilizofuta na
zote wapinzani walishindwa, na hata safari hii CCM itashinda.
Akimgeukia
Lowassa, Nape alisema Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu, amedanganywa na
wapambe wake na kuondoka chama tawala, na kwamba licha ya kuhamia huko,
CCM itamshinda asubuhi na kuwataka wanaotishia kukihama kufanya hivyo na
si kuleta shinikizo.
“Katika
mchakato wa uchaguzi si wote watakaoridhika na matokeo kwa sababu kuna
wengi wanajiandaa kushinda na sio kushindwa, na matokeo yanapokuwa
hivyo, wanakuwa hawaridhiki na hapo ndipo wanazungumzia kwenda upande wa
pili, na hasa kwa shinikizo la wapambe.
“Hili
limetokea kwa Edward, amekwenda upande wa pili, amedanganywa na watu,
tutampiga. Ushindi wa CCM ni wa uhakika, sio wa matumaini. Matumaini
yapo Angaza, CCM ni ya uhakika. Tutashinda asubuhi. Tumesema ni mpambano
kati ya wagombea na makapi,” alisema Nape na kuongeza:
“Zipo
mechi ambazo unajua hii utashinda. Yanga na Lipuli ya Iringa unajua
matokeo yake. Tunataka mgombea mwenzetu apelekewe ambulance (gari la
wagonjwa) nyumbani kwake, kwani ushindi kwetu ni uhakika.
”
Kuhusu wanaolalamika na kutishia kuhama, alisema malalamiko hayawezi
kutolewa barabarani kwani chama hicho kina utaratibu wake na yale yote
yaliyolalamikiwa yakiwamo ya udiwani, yamefanyiwa kazi.
“Tulisema
wakati ule wa mchakato wa kutafuta mgombea wa urais kuwa hatutafanya
kazi kwa shinikizo. Tunajua uimara wa chama chetu, kama kuna watu
wanataka kwenda upande wa pili waende. Lakini CCM haiwezi kufanya kazi
kwa vitisho na shinikizo.
"Tatizo
ni kwamba kunatokea wagombea 12, halafu unasema lazima uwe wewe. Kuna
watu (wanaotaka kuhama) wanafanya hivyo kwa shinikizo la viroba na
hela,” alisema Nape.
~Mpekuzi blog
Post a Comment