Mwenyekiti
wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe amekata rufaa Mahakama Kuu kupinga
hukumu iliyotolewa dhidi yake Julai, mwaka huu, na kumtoza faini ya Sh1
milioni baada ya kupatikana na hatia katika kosa la jinai.
Mbowe
alitozwa faini ya Sh1 milioni au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela
kwa kosa la kumshambulia mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu wa 2010
katika Wilaya ya Hai, Nassir Yamin.
Hata
hivyo, Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) na Mbunge wa Hai, alilipa faini hiyo na kuachiwa huru
na Mahakama ya Wilaya ya Hai.
Katika
rufaa hiyo namba 33/2015, iliyofunguliwa na wakili Peter Kibatala,
Mbowe anailalamikia mahakama iliyomtia hatiani kuwa ilishindwa
kushughulikia hoja muhimu katika kufikia uamuzi huo.
Pia,
Mbowe analalamika kuwa mahakama ilishindwa kupima ushahidi kwa usahihi
na pia, ilishindwa kutilia maanani ushahidi wa mashahidi wa upande wa
utetezi akiwamo yeye.
Mbowe
analalamika kuwa mahakama ilishindwa kutumia msingi wa jukumu la
kuthibitisha shitaka pale ilipoeleza kuwa mashahidi wa upande wa
mashtaka walitoa ushahidi uliojitosheleza.
Kwa
mujibu wa Mbowe, Mahakama hiyo ilitakiwa itumie dhana ya upande wa
mashtaka kuwa unatakiwa uthibitishe shtaka bila kuacha mashaka, jambo
ambalo halikufanyika.
Mkata
rufaa huyo anailalamika pia mahakama hiyo ilishindwa kueleza sababu
zilizoifanya ifikie uamuzi wake huo kama inavyoelekezwa katika sheria ya
mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka
2002.
Kutokana
na sababu hizo, Mbowe ameiomba Mahakama Kuu kuifuta hukumu iliyomtia
hatiani, kurejeshewa Sh1 milioni alizolipa kama faini na apewe nafuu
nyingine yoyote ambayo mahakama itaona inafaa.
Rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa Septemba 2, mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari.
Post a Comment